Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dullah Mbabe: Ngumi iliyomzimisha Cheka niliifanyia mazoezi siku 30

Dullah Pic Data Dullah Mbabe: Ngumi iliyomzimisha Cheka niliifanyia mazoezi siku 30

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

ALIPOMCHAPA kwa knock out (KO), Francis Cheka maneno yalikuwa mengi. Wapo walioamini kabahatisha, lakini wengine walisema amemkuta Cheka ndiyo anaishia kwenye masumbwi.

Ilikuwa Desemba 26, 2018, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ alipomchapa Francis Cheka kwa KO kwenye Ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Kwenye pambano hilo la ubingwa wa WBF wa mabara la uzani wa super middle, sio mashabiki wa Cheka tu ambao hawakuyatarajia matokeo hayo, lakini hata Cheka mwenyewe alisema hakujua nini kimemkuta.

“Ile ngumi inaitwa ‘aliyeenda kaenda’. Niliifanyia mazoezi kwa siku 30 ndiyo sababu ilimletea madhara Cheka ilipomkuta,” anasimulia Mbabe katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Anasema alipoletewa ofa ya pambano hilo, kwanza alirudi nyuma kutokana na uwezo wa Cheka wakati ule.

“Katika ngumi za Tanzania, Cheka sio bondia wa kumchukulia poa kabisa kama watu walivyomchukuliwa baada ya kuwa nimempiga KO.”

Mbabe anasema alipata ujasiri wa kucheza pambano hilo kutokana na historia yake ya kutokuwa na woga hasa wa kupigana na mabondia wakubwa nchini.

“Wakati huo nilikuwa na rekodi ya kumpiga Maneno Oswald aliyekuwa tishio, Mada Maugo, Said Mbelwa na Thomas Mashali (sasa ni marehemu).

“Nilipoletewa ofa ya kupigana na Cheka nikasema nacheza,” anasema Mbabe.

“Nilianza kufanya mazoezi ya kucheza na Cheka, nakumbuka ngumi iliyomzimisha ilikuwa ya kulia ambayo niliifanyia maozezi muda mrefu sana, si chini ya siku 30.

“Kocha wangu wakati ule Shomari Kimbau alikuwa alihakikisha kila siku naifanyia mazoezi na kweli kwenye pambano nilipoiachia ilimkuta Cheka kwenye shavu.

“Lilikuwa kombora zito, lilimkuta moja kwa moja ndiyo sababu hakunyanyuka kwa kuwa niliifanyia mazoezi ya kutosha, lakini narudia tena kwenye ngumi za kulipwa nchini Cheka si bondia wa kumbeza.”

Anasema kilichombeba kwenye pambano hilo ni ujasiri, kwani amekuwa hana hofu katika maisha yake ya ngumi kucheza na mabondia wakubwa nchini.

“Kuna mwaka niliwahi kwenda China kucheza kwenye mashindano ya Bingwa wa Mabingwa, nikiwa bondia pekee kutoka Tanzania, nilipigana na bondia Mrusi, huyu ndiye alinijenga na kunifanya kutohofu kucheza na bondia yoyote yule,” anasimulia mwanamasumbwi huyo.

HATaMSAHAU MASHALI

Katika miaka 17 ya Mbabe ulingoni tangu akiwa kwenye ngumi za ridhaa hadi sasa anacheza ngumi za kulipwa, anasema hawezi kumsahau Thomas Mashali.

“Kuna pambano nilicheza naye, mashabiki wangu walipigwa mabomu ya machozi baadhi yao wakazimia.”

Mbabe na Mashali wamewahi kuzichapa mara mbili, ambapo awali ilikuwa Januari Mosi, 2015 kwenye Ukumbi wa Friends Corner jijini Dar es Salaam katika pambano la raundi nane.

Mwamuzi Sakwe Mtulya hakumtangaza mshindi baada ya majaji Said Chaku, Fidel Haynes na Ibrahim Kamwe kutotoa matokeo.

“Hilo ndilo lilikuwa pambano langu kubwa kwenye ngumi za kulipwa, nilipoletewa mkataba nilijipa moyo sababu katika vitu nilivyobarikiwa ni kutokuwa mwoga.

“Nikiwa bondia wa ridhaa na timu ya Ngome nilicheza mechi 40 bila kupoteza na niliwahi kwenda kwenye mashindano ya majeshi nchini Uganda nikiwa na timu ya Ngome huko nilijengwa sana ukakamavu,” anasema Mbabe.

Anasema alipohamia kwenye ngumi za kulipwa alikuwa na shauku ya kuzichapa na Mashali ambaye wakati huo alikuwa staa nchini.

“Nilitaka nionekane, hivyo nilipopata nafasi hiyo nilisema sitafanya makosa. Pambano hilo liliisha kwa vurugu ila nilimpiga.

“Wakati ule ngumi hazikuwa na ustaarabu kama sasa. Tulicheza Manzese ambako ni nyumbani kwao Mashali, tulimaliza raundi zote nane, lakini nilimpiga matokeo hayakutangazwa kwa kuwa

kulitokea vurugu kubwa.

“Mashabiki wangu baadhi walizimia, kwani yalipigwa mabomu ya machozi kusambaratisha watu sijapata kuona. Sasa hivi ngumi zimestaarabika zinachezwa Masaki, ni jambo la kumshukuru Mungu,” anasema.

Mbabe anasema baada ya pambano hilo ndipo akaanza kupata jina japo halikuwa na mshindi. Machi 15, mwaka huohuo wakaandaliwa pambano la marudiano lililopigwa kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Mabondia hao walicheza raundi zote 10 na mwamuzi Anthony Ruta kumtangaza Mbabe kuwa mshindi baada ya jaji Said Chaku kumpa pointi 99-91, Robert Kasiga kutoa pointi 97-93 na Pembe Ndava kutoa 95-95.

“Mashali ndiye bondia aliyenitambulisha kwenye ndondi za kulipwa nchini, pambano dhidi yake ndiyo lilinipa umaarufu.”

AJUTIA PAMBANO

Novemba 11, 2019, Mbabe alichapwa kwa KO na Rocky Fielding nchini Uingereza katika pambano ambalo Mtanzania huyo anasema anajutia. “Nilitegemea liwe pambano ambalo lingebadilisha maisha na rekodi yangu kwenye ngumi, lakini presha ilikuwa kubwa nikajikuta nimelipoteza,” anasema.

Mbabe alizichapa na bondia namba tano wa dunia - pambano ambalo kama angeshinda lingevunja rekodi ya lile la Hassan Mwakinyo na Sam Eggington aliyekuwa bondia namba nane wa dunia.

“Nilipigwa kihalali kabisa, hakukuwa na figisu zozote,” anaeleza Mbabe akisimulia matokeo ya pambano hilo lililopigwa Olympia jijini Liverpool nchini humo.

Anasema pambano hilo kwake lilikuwa na presha, na kwamba alitamani apate ushindi ambao aliamini utamfikisha katika kiwango tofauti.

“Nilipigwa kihalali, hakuna namna gani vipi ambayo ilifanyika, nilipanda ulingoni nikiwa na presha kubwa. Hicho ndicho chanzo cha kupigwa.

“Mpinzani wangu alikuwa bondia mkubwa sana duniani, japo kingine kilichonigharimu ni kwamba kwenye pambano lile nilipokea mkataba ukieleza nitacheza kwenye uzani wa super middle kilo 76.2.

“Nikiwa kule uzani ukabadilishwa. Nikatakiwa kupigania light heavy, kidogo ikanipa changamoto kwa kuwa nilijiandaa kucheza super middle,” anasema.

Mbabe anasema kama angecheza uzani halisi huenda pia asingepoteza kwa KO pambano hilo kwa kuwa alifanya maandalizi ya uhakika na alikwenda London mapema.

“Nilikaa kule kwa siku zisizopungua 10 nikiwa kwenye maandalizi, nakumbuka kama siku zisizopungua 10 nilijifua kwenye gym nzuri yenye kila kitu.

“Mazingira yalikuwa mazuri, chakula nilipata kwa wakati muafaka - tena aina yoyote niliyohitaji, nilipewa usafiri binafsi kutoka London kwenda Liverpool ambako pambano lilikuwa likichezwa.

“Nililipoteza kwa kuzidiwa tu kwa kuwa mpinzani wangu alikuwa ni bora, hakukuwa na figisu zozote.”

UBINGWA WA DUNIA, REKODI

Agosti 30, 2019, Mbabe alitwaa ubingwa wa dunia wa World Boxing Organisation Asia Pacific nchini China. Katika pambano hilo alimchapa Zulipikaer Maimaitiali na kuweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza kumchapa mwanamasumbwi ambaye hakuwa amewahi kupigwa katika mapambano 12.

Pambano hilo lilipigwa kwenye ukumbi wa TSSG Center, Qingdao na Mbabe kushinda kwa technical knock out (TKO) kwenye uzani wa super middle. “Wakati ule ngumi nilikuwa nazitamani sio kama sasa tunacheza cheza tu kwa kuwa hatuna pesa, hivyo tunapigana sababu ya ‘njaa’,” anasema.

“Nakumbuka ile ‘fight’ ya China nilicheza kwa ari na nguvu zote binafsi promota akinivuruga na mimi namvuruga, ila nawashauri mabondia msiwe wagomvi, ngumi sio ugomvi ni mchezo kama michezo mingine.”

TUHUMA ZA KUUZA MAPAMBANO NJE YA NCHI

Kumekuwa na tetesi za mabondia nchini kutuhumiwa kuuza mapambano wanapokwenda kuzichapa nje ya nchi.

“Matukio hayo kwenye ngumi hayakosekani, kwani kila kitu kina mitihani yake, hivyo hata kwenye ngumi hiyo ni sehemu ya mitihani,” anasema.

“Matukio hayo yapo na yanafanyika, lakini wakati mwingine bondia unatakiwa kujua malengo yako ni nini, ujiulize unapokabidhiwa bendera ya taifa maana yake ni nini? Unapokumbana na tukio la kushawishiwa kuuza pambano inabidi uubebe uzalendo.”

KUHUSU PAMBANO NA KIDUKU

“Watanzania wakae mkao wa kula, tayari mkataba umesainiwa na pesa tumekula, hivyo Juni lazima nilipe kisasi,” anasema Mbabe akizungumzia pambano la marudiano na Twaha Kassim ‘Kiduku’. “Bila shaka ‘fight’ ya tatu itakuwa Juni, nafahamu mashabiki wangu waliumizwa mno na pambano la awali, lakini safari hii niwambie tu kwamba Mungu yupo.

“Sikuhujumiwa, nilipigwa kihalali ila narudia tena, sasa hivi Mungu yupo na itajulikana kama kachumbari ni mboga au huwa inasaidia siku za shida tu,” anasema bondia huyo anayejifua kila siku kwenye gym ya Makumbusho chini ya kocha Omari Dame Perege.

SAFARI YA MIAKA 17 ULINGONI

Mbabe aliyeanza ngumi 2004 akiwa na timu ya Ngome, anasema alipigana kwenye ngumi za ridhaa mara ya kwanza na Ramadhan Kido na kushinda “Ila zimenilipa namshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na mazingira niliyopo sasa na nilipotoka, ngumi zimenisaidia sana.

“Nilipigana mapambano 40 bila kupoteza, nikaona sasa nimeiva kujiunga na ngumi za kulipwa mwaka 2013 ndipo nilicheza pambano langu la kwanza na Seleman Mausa na kushinda kwa RTD ikiwa ni Desemba 31.”

Tangu wakati huo, Mbabe alianza kujulikana kwenye renki ya dunia na mpaka sasa ni bondia wa 189 kati ya 1,220 duniani na wa kwanza kati 15 nchini katika uzani wa super middle, amepigana mapambano 39, ameshinda 29 (26 kwa KO), amepigwa mara 9 (2 kwa KO) na kutoka sare mara moja.

Hata hivyo kwenye orodha ya mabondia wote nchini (Pound for Pound), Mbabe ambaye alikuwa kwenye tano bora ameporomoka.

“Ni kweli nimeporomoka, kwenye renki lakini bado katika orodha ya mabondia ambao wanakubalika nchini nimo, iliwahi kuzungumzwa kwenye orodha ya walioiwakilisha vema nchi na mimi nimo. Ni bondia pekee ambaye nimechukua ubingwa wa dunia nikiwa nje ya nchi kwa kizazi hiki na Ibrahimu Class (alishinda ubingwa wa dunia wa GBC nchini Ujerumani).”

HUMWAMBII KWA BONDIA HUYU

“Akiwa anapigana kwanza lazima uvute kiti ukae utulie umwangalie tu, ni bondia pekee ambaye anajua ngumi hapa nchini,” anasema Mbabe akimtaja Nasibu Ramadhan.

Nasibu alianza kupigana kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2009, ni bondia wa 79 kati ya 1,130 duniani na wa tatu katu ya 47 nchini kwenye uzani wa super bantam, amecheza mapambano 49, ameshinda 31 (18 kwa KO), amepigwa mara 16 (4 kwa KO) na kutoka sare mapambano mawii.

“Namkubali Nasibu ni fundi wa ngumi nchini, anazijua ngumi na zenyewe zinamjua akiwa anacheza lazima utafute kiti ukae kwa utulivu uangalie ladha ya ‘boxing.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz