MABONDIA, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kiduku, leo watachuana katika pambano la raundi 12 la kuwania mkanda wa taifa uzito wa kati wa kilo 76.5.
Pambano hilo litapigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na linatarajiwa kushuhudiwa na mamia ya mashabiki.
Pazi na Kiduku wamepaniana, ambapo kila mmoja ametamba kuwa ndiye mwamba baada ya jana kupima uzito na kushindwa kuficha hisia zao wakitaka kuonyeshana kazi mapema.
Tangu kutangazwa kwa pambano hilo kila mmoja alikuwa akifanya maandalizi yake na leo itajulikana ni nani aliyejiandaa vizuri.
Rekodi zinaonesha mara ya mwisho walikutana 2017 na kutoka sare, ingawa Kiduku hakukubali matokeo hayo,akidai mwenzake alibebwa na majaji na kuomba kukutana tena.
Wakizungumza baada ya kupima uzito jana, Pazi alisema hajui nini kitakachomkuta mpinzani wake, kwani amejiandaa vizuri kummaliza mapema.
“Tukutane kesho (leo) pale Uhuru, nitamuua Kiduku, nimejiandaa vizuri naamini nitashinda,” alisema.
Naye Kiduku alisema ushindi kwake ni kawaida wala hana wasiwasi katika pambano hilo.
“Nadhani Dulla Mbabe ananitambua vizuri kwa hiyo kushinda kuko pale pale, nimejipanga na najiamini kuwa nitashinda,” alisema.
Pazi ni mzoefu zaidi kuliko mpinzani wake, kwani amecheza mapambano 35 na kati ya hayo ameshinda 27, huku 24 ni kwa ‘knockout’, akipoteza saba na kupata sare moja na Kiduku amecheza mapambano 22 na kati ya hayo ameshinda 15 na nane kwa ‘knockout’, amepoteza sita na sare moja.
Atakayeshinda pambano hilo atatangazwa kuwa mfalme wa Wazaramo, kwani wote wawili ni kama ndugu kikabila ingawa hawajuani na wanakutana katika kazi hiyo.
Kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi kabla ya pambano la wababe hao, ambapo Nassibu Ramadhan atachuana na Ibrahim Class, Paul Kahata dhidi ya Hussein Haba, Ramadhan Joncina dhidi ya Habibu Pengo na Stumai Miki dhidi ya Agnes Kayage.
Muandaaji wa pambano hilo, Jay Msangi, amewahimiza mashabiki wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi kujaza Uwanja wa Uhuru ili kuwaunga mkono mabondia hao.