"Ili kufanya mazoezi, ilikuwa lazima twende kuomba ruhusa kwa Shekha, huko ndipo tulipewa kibali maalumu kujifua, hata hivyo ugumu zaidi ukawa ni kwenye kucheza.
“Mabondia kutoka Zanzibar iliitubidi kutoa hela ili tununue mapambano tucheza kule Bara, tulifanya hivyo tukilenga kujiweka katika renki na kujulikana Boxrec (mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia),” anaanza kusimulia bondia wa zamani ambaye sasa ni kocha, Salum Juma.
Salum ambaye alianzia kwenye ngumi za ridhaa, ambazo anasema wakati huo alivuka maji na kwenda Dar es Salaam kupigana, kabla ya kuhamia kwenye ngumi za kulipwa, kote huko amepigana Zanzibar ikiwa imepiga marufuku mchezo huo.
Ndondi zilipigwa marufuku na Rais wa kwanza, Abeid Amaan Karume, ingawa kumekuwa na maelezo tofauti kuhusu marufuku hiyo ambayo wengine wanasema ulionekana kama mchezo wa unyama, yakichukulia mapigano yalikuwa ni ya wanyama.
“Tumekuta vitu vingi vinazungumzwa kuhusu marufuku hiyo, wengine wanasema alipigwa mtu akavunjika mbavu, wengine wanasema mabondia walikuwa ni wahuni na walipigana kavu kavu mitaani, ndipo Rais wa enzi hizo (Abeid Karume) akaamua kuufungia,” anasema bondia huyo mkongwe.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine ambaye pia marufuku hiyo aliikuta, anasema historia inaonyesha zamani ulichezwa bila kufuata sheria ikiwamo ya uzito na nyinginezo.
“Ulionekana ni mchezo wa hatari, Rais wa wakati ule akaufungia, baadae ikaanzishwa kickboxing na mashabiki wengi walijitokeza kuangalia, lakini ukapigwa marufuku hivyo mwamko ukaendelea kuwepo kwa mabondia kujifua na kwenda kucheza Bara.
“Alipoingia madarakani DK Mwinyi, ilionekana ipo haja ya kulitizama hili upya, ilipelekwa hoja Baraza la Wawakilishi, kisha Baraza la Mapinduzi ambao waliamuru ufanyike utafiti kuona ni jinsi gani mchezo huo utarudi.
“Asilimia 65 walisema uchezwe, wanawake wakiwa ni wengi zaidi wakitaka ngumi zirudishwe kuchezwa Zanzibar, Mheshimiwa mwenyewe alipitisha katika Baraza la Mapinduzi na ngumi zakarudishwa Zanzibar,” anasema.
Anasema baada ya kuondolewa marufuku hiyo, BTMZ ilikuja na miongozo ikiwamo kuwepo kwa kamisheni ambayo hivi karibuni itafanya uchaguzi wao baada ya uongozi wa muda.
Anasema Novemba na Desemba kutakuwa na mapambano mengi, ingawa kama Baraza la Michezo wanaelekeza nguvu kwenye ngumi za ridhaa ambako ndipo kuna vipaji.
MWINYI ABADILI UPEPO
Juma anasema kipindi chote ambacho mchezo huo ulipigwa marufuku Zanzibar, mabondia waliendelea kucheza akiwamo yeye kwa nyakati tofauti.
“Tulikuwa tukifanya mazoezi kwa kujificha, nyumbani kwetu kulikuwa na ringi tumefunga kwa ajili ya mazoezi, lakini ili tujifue tulienda kuomba kibali kwa shekha (balozi) na kujieleza sisi ni watoto wa mtaani tunapenda ngumi, tukawa tunaruhusiwa hivyo.
“Lakini kinyume na hivyo, ilikuwa ukionekana unashiriki ngumi unakamatwa, tulienda hivyo hadi tukatengeneza majina, lakini kwa kuomba kucheza mapambano Bara, wakati mwingine tunamlipa bondia wa kule ili tupate fursa ya kucheza.
“Tulikuwa tukicheza ngumi kwenye mazingira magumu, japo ni mchezo ambao binafsi umenipa mafanikio, nimejenga na kusomesha wanangu kupitia ngumi,” anasema Juma ambaye sasa ni kocha maarufu wa mchezo huo visiwani Zanzibar.
Agosti 27, kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50 ya marufuku ya ndondi zilipigwa kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung , Rais, Dk Hussein Mwinyi ndiye alikuwa mgeni rasmi akiwashuhudia mabondia wa Zanzibar wakitoana jasho na wale wa Bara.
Mabondia hao ni Musa Nassor (Banja) aliyecheza na Abdallah Pazi (Dullah Mbabe), Osman Muller Junior aliyecheza na Karim Mandonga na Hamis Muy Thai aliyezichapa ngumi kwa mara ya kwanza dhidi ya Ibrahim Class akitokea kwenye kickboxing.
Uwanja huo ulifurika wake kwa waume, kushuhudia mtanange huo, ambao ulifanyika baada ya Dk Mwinyi kuondoa marufuku hiyo na kuruhusu masumbwi kuchezwa tena visiwani humo. “Rais wetu alijionea mwamko ulivyokuwa mkubwa, kifupi ameturejeshea fursa ambayo tuliipoteza, aliona Zanzibar ilivyo na vipaji vya ngumi, Mandonga alikuja huku na kachapika.
“Mwenyezi Mungu azidi kumpa maisha marefu Rais wetu kwa jinsi anavyotuongoza na sisi tunamuahidi hatutomwangusha,” anasema.
MABONDIA ZENJI NI MDEBWEDO
Kocha huyo anasema kurejeshwa kwa mchezo huo kumetoa fursa nyingi si tu kwa mabondia wanaume, hadi wanawake visiwani humo na sasa wameanza kujikita kwenye ngumi.
“Kuna maneno tumekuwa tukiyasikia kutoka Bara mabondia wa Zanzibar ni mdebwedo (hawana nguvu), atakayevuka maji kuja huku kucheza kabla ya kupima uzito apitie Malindi kwanza akatizame mazingira ya kule yalivyo ndipo waje ulingoni.
“Wasituchukulie wepesi, huku hawatoki, tumejipanga na sasa vijana wanajifua kwa kiwango bora kufanya vizuri, kama tuliwatoa jasho wakati wa marufuku, safari hii tunajifua muda wote wajiandae kukalishwa,” anasema.
Mabondia hao wanajifua kwenye gym maarufu iliyopo Zan City na kocha huyo anasema wana ratiba ya mazoezi asubuhi kuanzia saa 2 ahi saa 5 kila siku.
KLABU 48 ZASAJILIWA
Katibu wa Kamati ya Ufundi na Mashindano kwenye Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Zanzibar (ZaPBC), Hamis Said Seif (Mkali Swahiba) anasema tangu Rais Mwinyi ameondoa marufuku na kuruhusu ndondi kuchezwa visiwani humo, kuna klabu 48 zimesajiliwa.
“Mabondia ni wengi sana hapa Zanzibar, ukiachana na klabu hizo, pia kuna wanawake 15 katika kipindi hiki kifupi wanacheza ngumi, wanaume ni wengi zaidi, pia kuna wazungu nao wanapenda na tunao hapa gym wanajifua.”