Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cheka aahidi kuisimamisha Morogoro

100975 Cheka+pic Cheka aahidi kuisimamisha Morogoro

Tue, 11 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati mashabiki wakihesabu siku kushuhudia kile ambacho bondia Francis Cheka amewaahidi, bondia huyo anaamini pambano lake la Eid pili litasimamisha shughuli katika baadhi ya maeneo mkoani Morogoro linakopigwa.

Cheka atazichapa na Shaban Kaoneka kwenye uwanja wa Jamhuri, pambano la raundi 10 lisilo la ubingwa.

Zikiwa zimepita zaidi ya siku 800 bila bondia huyo bingwa wa zamani wa dunia wa WBF kupanda ulingoni, mashabiki wake watamshuhudia kwa mara nyingine akizichapa na Kaoneka bondia pekee aliyewahi kumpiga kwa KO Hassan Mwakinyo.

"Ni pambano ambalo kwangu lina mambo matatu, kwanza kuthibitisha ubora wangu kwa mashabiki, kushinda na kunitambulisha upya kwenye ramani ya ngumi," amesema Cheka.

Amesema kwa namna mashabiki wake mkoani Morogoro na kote nchini walivyompokea baada ya kutangaza kurejea tena ulingoni, hana shaka atakuwa na muendelezo mzuri na pambano lake la Eid Pili litakuwa gumzo.

"Mashabiki wamehamasika, tangu nilipokuja kuweka kambi hapa Morogoro baada ya kurejea kutoka nchini Msumbiji (alikokuwa akiishi tangu 2018 mwisho), hamasa imekuwa kubwa, wengi wanatamani kuniona upya ulingoni.

"Nawaahidi sitowaangusha, hiki ndicho kipimo changu kwenye ngumi kwa mara nyingine, kama Kaonekana atamaliza raundi zote 10, basi nitajua nahitaji kujifua zaidi," amesema.

Endapo atashinda pambano hilo, Cheka ameahidiwa kuletewa bondia kutoka nchini Cameroon ambaye atazichapa naye jijini Arusha pambano la ubingwa.

"Nasisitiza tena niko vizuri, sijarudi ulingoni kwa bahati mbaya, japo ile kasi ya mwanzo itapungua, lakini ufundi na uzoefu ninavyo vya kutosha," amesema.

Pambano la Cheka na Kaoneka litaanza saa 9 Alasiri na linatarajiwa kumalizika saa 12 jioni likitanguliwa na mengine matano.

Mabondia hao watapima uzito na afya siku ya Eid Mosi, ingawa Kaonekana amemtahadharisha Cheka akisisitiza kuwa asitarajie kutoka tena kwenye ngumi kupitia yeye Kaoneka.

"Nafahamu Cheka Morogoro ana mashabiki wengi, licha ya kuwa na nguvu hiyo, lakini nitamnyamazisha yeye na mashabiki wake," alijinasibu Kaoneka.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz