Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bondia Mandonga aibuka na Ukraine staili

Mandonga Ndondo Karim 'Mandonga' Said

Fri, 13 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Achana na ngumi ya ndoige, keshokutwa Jumamosi, Karim 'Mandonga' Said anakwambia atakuwa na staili mpya kabisa ambayo hamuifahamu atakapocheza pambano lake la kwanza la kimataifa nchini Kenya.

"Kiwango kimepanda, lazima nije kwa staili ya tofauti," anasema bondia huyo ambaye tayari yuko nchini Kenya akijiandaa kuzichapa na mwenyeji, Denzel Onyango Okoth pambano la raundi 10.

Pambano hilo linaweza kuwa 50/50 na bondia mwenye bahati na mbinu za kiufundi kati yao ndiye ataibuka shujaa kwenye dakika 30 wanazotarajiwa kucheza ndani ya ukumbi wa Charter, jijini Nairobi.

"Safari hii mashabiki wangu wajiandae kuona ngumi za kimataifa, kuna ngumi inaitwa Ukraine staili, hii ndiyo itakayomsulubu Okoth," alijinasibu Mandonga.

MANDONGA NI NANI? Bondia huyu namba tano kwa ubora kati ya mabondia 31 wa uzani wa middle nchini Tanzania ana rekodi ya kucheza mapambano saba, amepigwa mara tatu kwa Knock Out (KO) na kushinda mara tatu (2 kwa KO) na sare moja ana uzoefu wa miaka minane ulingoni.

Nchini, Mandonga ni kipenzi cha mashabiki wengi kutokana na tambo zake za nje ya ulingo ambazo siku za karibuni mwenyewe anasema si tambo tu na vitendo vinafanyika.

"Nilimwambia Alibaba (Ramadhan alicheza naye pambano la mwisho hivi karibuni na kushinda kwa pointi), Mandonga mtu kazi sina kazi mbovu, nikamuonyesha nilichokimaanisha.

"Huyu Mkenya pia anafuata nyayo, sasa niko anga za kimataifa, siwezi kucheza ngumi kama nilizokuwa nikicheza nyumbani, huku nitacheza Ukraine staili, bila shaka ubora wa mabondia wa Ukraine unafahamika, hivyo Kenya wajiandae kushuhudia ngumi za levo nyingine," anajinasibu Mandonga.

Bondia wa uzani wa juu, Oleksandr Usyk anayekamata namba sita duniani kwa ubora kwenye kila uzani ni miongoni mwa nyota kutoka Ukraine wanaotamba kidunia.

Licha ya tambo hizo, Mandonga atahitaji ufundi na mbinu zaidi kumchapa Okoth bondia chipukizi mwenye uchu na ushindi ambaye hawezi kuruhusu rekodi yake ya kutopigwa ivunjwe nyumbani.

Okoth ana miezi 10 tu kwenye ngumi za kulipwa, amepigana mara mbili na kushinda kwa Technical Knock Out (TKO), awali alimchapa Denis Otieno raundi ya pili, Machi 2 mwaka jana, miezi saba baadaye akapata matokeo kama hayo raundi ya kwanza dhidi ya Mussa Omary Nassor.

"Mtu kazi nakwenda kutibua rekodi yake, nimejipanga na ninahitaji kuweka heshima, nimefanya mazoezi kwa kiwango bora, nilibadili ratiba yangu nzima ya mazoezi na kujifua siriazi, siko tayari kupoteza pambano hili ambalo lina maana kubwa kwangu.

"Kwanza ni la kimataifa, napigana kwa mara ya kwanza kwenye levo hizo, pia nacheza na bondia ambaye hajawahi kupigwa, tena akiwa kwao, hii nafasi siifanyii makosa," anatamba.

Mandonga atapanda ulingoni akiwa mzoefu zaidi, japo hakuwa na muendelezo mzuri tangu Juni, 26, 2015 alipocheza pambano lake la kwanza na kuchapwa kwa Knock Out (KO) na Benki Mwakalebela, pambano ambalo lilianza kurudisha umaarufu wake.

Miaka sita baadaye, Agosti 14, 2021 ndipo alishinda kwa mara ya kwanza alipomchapa kwa pointi Omari Mgoa, kabla ya kuendeleza rekodi ya kupigwa, japo hivi karibuni ameshinda mara mbili mfululizo.

Pambano lake la Julai 30, 2022, ndilo lilimtoa na kuanza kukubalika kwa mashabiki licha ya kuchapwa na Shaban Kaoneka, tambo na maneno yake ya vitisho kabla na baada ya pambano ndiyo vilimpa umaarufu na kuanza kukubalika kwa mashabiki nchini.

PAMBANO LA KUSHTUA Novemba 25, mwaka jana, Mandonga aliandika rekodi mpya iliyowashtua wengi ikiwemo mabondia nchini baada ya kumchapa Said Mbelwa, kwa TKO.

"Wakati naingia kuchezesha pambano hilo, akili yangu yote ilikuwa ni kumlinda na nilijipanga kuwahi kumuokoa Mandonga ili asidhurike nikiamini ubora, rekodi na uwezo wa mpinzani wake, Mandonga atachapika hasa lakini ikawa ndivyo sivyo" anasema aliyekuwa refarii wa pambano hilo, Anthony Rutha.

Anasema kilichomshtua ni namna bondia huyo alivyotawala mchezo kuanzia raundi ya kwanza hadi mwisho na kupata ushindi ambao ndiyo ulimpandisha kutoka nafasi ya 30 hadi ya tano kwa ubora nchini.

Bingwa wa zamani wa dunia wa mkanda wa WBF kwenye uzani wa Super Middle,, Francis Cheka anasema hakutarajia kumuona Mandonga kwenye ubora ule.

"Inaonekana amebadili hata mfumo wake wa mazoezi, si Mandonga yule ambaye tulimzoea kumuona akipigwa kama begi, yuko fiti, ana nguvu, ana timing, anajua ku-guard, kifupi yuko vizuri," anasema.

Alipozungumza na Mwanaspoti, bondia huyo alikiri kubadili ratiba ya mazoezi na kufanya mazoezi ya nguvu, yenye malengo na ufundi zaidi.

"Watu wengi walikuwa wakinidharau na kuona Mandonga Mtu Kazi ni mtu wa kupigwa, ila nataka niwaonyeshe walichokiwaza sicho, matamanio yangu ni kumvunja mtu taya au mbavu ulingoni ili heshima iwepo," anajinasibu bondia huyo anayekamata nafasi ya 442 kati ya 1465 duniani akimuacha kwa nafasi 70, Okoth ambaye ni wa 512.

Baada ya pambano la Kenya, Mandonga atakuwa na siku 12 za kupumzika kabla ya kupanda tena ulingoni Januari 27 kuzichapa na Nassor Abdallah.

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa anasema kucheza mfululizo kwa bondia huyo siYo tatizo, kama yuko fiti anapanda ulingoni.

"Yule ni mchezaji, akiona yuko fiti na amepata pambano, kama hajapigwa kwa KO au TKO, basi anacheza wala hakuna tatizo," anasema Palasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live