Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyechapwa KO na Kiduku, kuzichapa na Mwakinyo

Mbiya Kanku Mbiya Kanku.

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zikiwa zimebaki siku 20 kabla ya kupanda ulingoni, Hassan Mwakinyo amebadilishwiwa mpinzani safari hii akiletewa Mcongo, Mbiya Kanku bondia aliyewahi kupigwa Knock Out (KO) na Twaha Kiduku.

Awali, ilitangazwa Mwakinyo atazichapa na Mzimbabwe, Enock Msambudzi kabla ya leo kuelezwa atazichapa na Kanku, bondia mwenye rekodi kali zaidi ya Mzimbabwe aliyepangwa kuzichapa naye awali.

Kanku mwenye rekodi ya kushinda kwa KO katika mapambano yake yote 11 ya ushindi na kupigwa mara 6, ikiwamo tano wa KO na sare moja ni namba 169 kati ya 1,571 duniani na namba moja nchini kwake kwenye uzani wake.

Bondia huyo mwenye uzoefu wa miaka 10 ulingoni na nyota moja na nusu ni saizi ya Mwakinyo kwa sasa kutokana na kuendana kwa karibu rekodi zao za ndani na kimataifa.

Mwakinyo mwenye uzoefu wa ulingo kwa miaka minane ana nyota mbili na nusu akiwa nafasi ya 106 kati ya 1,935 duniani na namba moja nchini kwenye uzani wake akishinda mara 21 na kupigwa mara tatu.

Mabondia hao wametofautiana uzani, Kanku akipigania middle na Mwakinyo super welter, hivyo kwenye pambano lao Mwakinyo atalazimika kupandisha uzani au mpinzani wake kushusha.

Tofauti yao nyingine ni kwenye 'stance' Mwakinyo akitumia zaidi mkono wa kulia (orthodox) na mpinzani wake kushoto (southpaw) ambao ni wabishi kupigika kirahisi.

Mwakinyo atatakiwa kufanya kazi ya ziada kushinda Januari 27, watakapozichapa kwenye uwanja wa New Amaan, Zanzibar pambano la raundi 10.

Japo, Kanku amewahi kupigwa na Kiduku kwa Knock Out (KO) ya dakika ya 2:50 ya raundi ya tatu katika pambano lililokuwa la raundi nane lililochezwa Agosti 27, 2016 huko Lusaka, Zambia kwenye ukumbi wa Government Complex chini ya refarii, Maybin Kante.

Mwakinyo na Kiduku wamekuwa kwenye upinzani, mashabiki wakitamani kuona pambano hilo ambalo kwa zaidi ya miaka mitatu limeshindwa kufanyika huku 'team' zao zikitupiana vijembe.

Kambi ya Kiduku inaweza kuzungumza zaidi kama Mwakinyo atapoteza pambano hilo, jambo ambalo upande wa Mwakinyo hautarajii hilo litokee, huku hivi karibuni kukiibuka vijembe kwa pande hizo baada ya kauli ya Mwakinyo aliyoitoa kwamba yuko tayari kupigana na bondia yoyote ikiwamo huyo wa Morogoro ambaye hakumtaja jina.

Meneja wa Kiduku, Ibrahim Nyange alijibu mapigo akisisitiza kwamba mdomo hauchezi ngumi, bali mikono na pambano hilo wamekuwa wakilisubiri muda mrefu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live