Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Achana na sura, wanapiga ngumi balaa

CLARESSA SHIELDS (16).jpeg Achana na sura, wanapiga ngumi balaa

Wed, 3 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Masumbwi yamepata umaarufu mkubwa, yakivutia watu wa aina tofauti kuingia kwenye mchezo huo. Hakuna ubishi, masumbwi ni mchezo wenye upinzani zaidi.

Huko nyuma, masumbwi ulikuwa ukifahamika kama mchezo wa wanaume, lakini ilipofika karne ya 18, wanawake waliingia kwenye mchezo huo na kuonyesha nao ni kiboko kwa kupiga ngumi.

Mwaka 1993, Marekani iliruhusu mabondia wa kike na hapo Christy Martin akasainiwa kama bondia wa kwanza wa ngumi za kulipwa.

Tangu wakati huo, wanawake wamevamia kwa kasi kwenye mchezo huo wa ulingoni na kupata sifa kubwa, wakishinda mapambano makubwa na kuwa mabingwa wa dunia. Hii hapa orodha ya mabondia wa kike waliopata umaarufu mkubwa kwenye mchezo huo wa masumbwi.

14. MIA ST. JOHN

Alizaliwa Juni 24, 1967, Mia alikuwa bondia wa kulipwa na bingwa wa zamani wa super welterweight. Alikuwa akishikilia pia mikanda ya IBA na IFBA kwa uzito light na alikuwa bingwa wa taekwondo. Baada ya kustaafu masumbwi aliingia kwenye mitindo na biashara na alikuwa mtaalamu wa afya ya akili.

Alistaafu mwaka 2016 baada ya kutamba kwenye masumbwi kwa miaka 19, akipigana mapambano 65, ameshinda 49, kupoteza 14 na sare mbili.

13. NATASCHA RAGOSINA

Alishika chati za juu kwa mabondia wa kike kwa uzito wa super middle, Natascha ni bondia aliyestaafu na hakuwahi kupoteza pambano.

Bondia huyo wa Russia, aliweka rekodi ya kushikilia ubingwa kwa muda mrefu, alipokuwa na mkanda wa WBA uzito wa super middle na ule wa WBC kwa uzito huo huo wa super middle.

Natascha alimchapa kila mpinzani aliyepanda naye ulingoni kwenye maisha yake ya masumbwi. Alishinda mapambano 30 kati ya 30.

12. GISELLE SALANDY

Alianza masumbwi akiwa na umri wa miaka 13. Giselle alifahamika tangu mdogo kwamba atakwenda kuwa bondia matata kweli kweli. Hata hivyo, safari yake ya masumbwi haikuwa ndefu sana baada ya kupata ajali na kufariki dunia mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 21.

Alikuwa bingwa wa dunia wa uzito wa light-middle akishikilia mikanda IWBF, WIBA, WIBF, WBA, WBC na GBU na alikuwa hajapoteza pambano lolote kwenye masumbwi yake.

11. REGINA HALMICH

Regina Halmich haina mjadala ni mmoja wa mabondia mahiri kabisa wa kike duniani. Ni moja ya majina makubwa kwenye mchezo wa masumbwi. Bondia huyo wa Ujerumani ni moja ya waliopata mafanikio kwenye masumbwi ya dunia kutokana na rekodi zake za ulingoni.

Alistaafu akiwa na rekodi ya 54-1-1, ambapo mapambano 16 alishinda kwa Knockout. Regina ni bondia aliyeweka rekodi tamu kabisa kwa upande wa mabondia wa Ulaya.

10. CHRISTY MARTIN

Isingekuwa sawa kutaja orodha hii bila ya kujumuisha jina la Christy Martin, bondia matata kabisa kuwahi kutokea kwa upande wa wanawake.

Masumbwi yake ya kulipwa alipigana kuanzia mwaka 1989 hadi 2012, akishinda ubingwa wa WBC kwa uzito wa super welter mwaka 2009. Aliachana na masumbwi baada ya kushinda mapambano 49, kupoteza saba na kutoa sare mara tatu, huku mapambano 31 kati ya hayo, alishinda kwa knockout.

9. HOLLY HOLM

Holly Holm ni bingwa mara 18 wa dunia kwenye masumbwi na kitu kilichokuwa kinavutia kuhusu yeye ni ujuzi wake anapokuwa ulingoni. Alipachikwa jina la ‘The Preacher’s Daughter’, alishinda mkanda wa WBF uzito wa Light Welter na alikuwa bingwa wa dunia wa uzito wa Welter akiwa na rekodi ya 33-2-3, huku mapambano tisa akishinda kwa KO. Baada ya kuachana na masumbwi, aliingia kwenye mapigano ya ngumi za vizimba UFC.

8. ANN WOLFE

Katika kipindi chake cha ubondia, Ann Wolfe alikuwa mpiganaji wa kike aliyehofiwa sana na wapinzani wake. Aliingia kwenye masumbwi ya kulipwa mwaka 1998 na Ann alipata mafanikio makubwa katika mchezo huo, akiweka rekodi ya 24-1-1.

Moja ya mapambano yake ya kukumbukwa ni lile alilomchapa Vanda Ward kwa ngumi moja tu iliyomwangusha ulingoni na kushindwa kuendelea na pambano. Ngumi moja tu.

7. CECILIA BRAEKHAUS

Jina alilokuwa amepachikwa ni ‘First Lady’, na hakika Cecilia Braekhaus alikuwa mmoja wa mabondia mahiri kabisa wa muda wote waliowahi kutokea kwenye mchezo wa masumbwi. Bondia huyo wa Norway aliweka rekodi ya kuwa mpiganaji wa kike asiyepigika kwenye uzito wa welter na alikuwa bondi wa kwanza wa kike kupigana na kushinda mikanda ya WBA, WBC, IBF na WBO kwenye uzito tofauti. Rekodi yake ni 37-2 huku mapambano tisa akishinda kwa KO.

6. AMANDA SERRANO

Amanda Serrano ni bondia wa kuliwa, ambaye amekuwa akichanganya pia na sanaa ya mapigano na wakati mwingine akiingia kwenye mieleka.

Ni mmoja wa mabondia wenye mafanikio makubwa, akishinda ubingwa wa dunia wa uzito wa feather na alikuwa akiushikilia mkanda wa WBO tangu mwaka 2019 na mikanda ya WBC na IBO tangu 2021. Licha ya kuwa na umri mkubwa, zaidi ya miaka 34, bondia huyo raia wa Purto Rica bado ameonekana kuwa shupavu.

5. KATIE TAYLOR

Katie Taylor aliingia kwenye masumbwi ya kulipwa mwaka 2016, alipopigana kwenye pambano aliloshinda kwa TKO kwenye raundi tatu dhidi ya Karina Kopinska.

Hilo lilikuja baada ya kustaafu soka na kuamua kuingia kwenye mchezo wa masumbwi.

Alipokuwa kwenye soka, alipata nafasi ya kuchezea mechi 11 timu yake ya taifa ya Jamhuri ya Ireland kati ya mwaka 2006 na 2009. Ni bingwa wa dunia wa uzito wa light.

4. LUCIA RIJKER

Lucia ni mabondia wajuzi zaidi waliowahi kutokea kwenye mchezo huo kutokana na kupigana kwa akili nyingi. Alitambulika kama mwanamke hatari zaidi duniani kutokana na kile alichokuwa akiwafanya wapinzani wake walipokutana naye ulingoni.

Bondia huyo Mdachi alistaafu akiwa na rekodi ya 36-0, huku mapambano 25 akishinda KO. Alipohamia kwenye masumbwi ya mateke, rekodi yake ni 11-0 na ameshinda mataji manne ya dunia.

3. LAILA ALI

Laila Ali ni bondia wa zamani wa masumbwi ya kulipwa ambaye kwa sasa amegeukia kwenye masuala ya televisheni baada ya kustaafu masumbwi. Ni binti wa bondia mahiri wa vizazi vyote, Muhammad Ali. Alifuata nyayo za baba yake kwa kuingia kwenye masumbwi na kuwa tishio. Aliondoka kwenye masumbwi akiwa ameshinda mikanda ya WBC, WIBA, IWBF na IBA kwa uzito wa super middle na IWBF kwa uzito wa light heavy.

2. MARY KOM

Mary ni moja ya wapiganaji mahiri wa kike na moja ya wanamichezo mahiri wa muda wote huko India. Hakika, bondia Mary alikuwa matata ulingoni, ilikuwa shughuli pevu kukabiliana naye na kushinda mataji ya kutosha ya ubingwa wa dunia.

Alipachikwa jina la ‘Magnificient Mary’, akiwa bondia pekee kuwahi kushinda medali nane kwenye mashindani ya ubingwa wa dunia na mwanamke pekee kushinda ubingwa mara sita kwenye ngumi za ridhaa za ubingwa wa dunia.

1. CLARESSA SHIELDS

Kwenye namba moja, yupo gwiji wa masumbwi kwa upande wa wanawake, Claressa Shields. Claressa ni bondia matata kwelikweli kukabiliana naye kwenye ngumi za uzito wa light middle.  Ni bondia pekee kuwahi kushinda ubingwa wa dunia kwa madaraja manne tofauti mfululizo.

Staili zake za kupambana ndicho kitu kinachovutia wengi, ambapo ukiacha masumbwi amekuwa mahiri pia kwenye mchezo wa mieleka ya MMA.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live