Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

Nimefarijika kuipa ubingwa Mbeya- Kisoki

7d5415709a94a97187638b77d474743d Nimefarijika kuipa ubingwa Mbeya- Kisoki

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA, Juma Kisoki amesema anajisikia faraja kuipa ubingwa wa CRDB Taifa Cup timu ya Mbeya City kwa mara ya pili, akielezea hatua hiyo ni ya mafanikio katika taaluma yake.

Kisoki amekiongoza kikosi chake katika ushindi dhidi ya Temeke katika fainali ya michuano ya mpira wa kikapu ya CRDB Taifa Cup zilizomalizika Jumamosi iliyopita kwenye viwanja vya Chinangali mjini hapa.

“Vijana wangu walicheza kwa kufuata maelekezo niliyowapa na ndio maana tumeweza kuibuka washindi.” alisema.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo walikuwa timu ya Arusha.

“Mechi ilikuwa ngumu lakini tuliweza kushinda katika kota zote kipindi cha pili na kuulinda ushindi wetu hadi mwisho wa mchezo,” alisema Kisoki,ambaye pia aliipa ubingwa Mbeya City mwaka 2015, huku akiweka rekodi ya kushinda taji hilo mara tano, mara tatu akiwa kama mchezaji na mara mbili kama kocha.

Mbeya City waliwafunga Temeke kwa vikapu 68-55 katika mechi iliyokuwa na ushindani. Mechi hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi kadhaa akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi.

Naye kocha wa Temeke, Shendu Mwagala alisema wapinzani wao walistahili ushindi kwa sababu wachezaji wake walibweteka na ushindi walioupata katika kota za awali.

“Tulishindwa kuendeleza ubora wetu katika kota mbili za mwisho, wenzetu walitengeneza faulo na kuzitumia vizuri.”

“Pia walifunga pointi tatu muhimu (three points) za kutosha zilizowafanya watuzidi,” alisema Mwagala.

Katika hatua nyingine, kocha wa timu ya wanawake ya Temeke, Lucy Augustino alisema amefurahi kwa mara ya kwanza katika historia yake kuchukua ubingwa wa CRDB Taifa Cup.

Aliwaongoza vema Temeke kuwafunga wenyeji Dodoma kwa vikapu 46-36 katika mchezo mwingine wa fainali uliokuwa na ushindani.

“Sina la kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na wachezaji wangu kwa kujituma uwanjani,” alisema.

“Dodoma walitufunga katika hatua za makundi, lakini tulifanyia kazi makosa yetu na kufanikiwa kuja kuwafunga katika fainali,” alisema Augustino.

“Walikuwa na safu ngumu ya ulinzi ambayo ilitushinda katika mechi iliyopita, lakini tuliwawekea mkakati katika mechi yetu ya fainali na kufanikiwa kuwafunga,” aliongeza.

Augustino alikuwa kama kocha wa muda wa Temeke na ndani ya msimu mmoja amechukua ubingwa.

Washindi wa kwanza walipewa Sh milioni mbili kila mmoja na washindi wa pili walipewa Sh milioni moja na wafadhili, benki ya CRDB.

CRDB pia imetoa Sh laki mbili na medali kwa kila timu, vyeti vya ushiriki na fedha kwa wachezaji waliofanya vizuri, wakiwemo Rehema Silomba na Baraka Sadicki, waliochaguliwa wachezaji bora (MVP) kwa upande wa wanawake na wanaume na kila mmoja kuzawadiwa Sh laki tatu.

Pia benki hiyo pia imetoa msaada wa masomo bure (scholarship) kwa wachezaji 24 waliochanguliwa baada ya kufaya vizuri.

Akizungumza katika ugawaji zawadi, DK. Abbasi alisema Serikali inatambua umuhimu wa michezo na sanaa na ndio maana imeamua kujenga uwanja wa kisasa mjini hapa ili kuendeleza michezo na wasanii.

Pia aliishukuru CRDB kwa mchango wa kusaidia vijana kupitia michezo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Mussa alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na taasisi nyingine katika kusaidia sekta ya michezo na shughuli za kijamii, huku akiahidi makubwa katika mashindano ya mwakani.

Chanzo: habarileo.co.tz