Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

NBA MVP yaacha gumzo Marekani

Mvp Pic NBA MVP yaacha gumzo Marekani

Tue, 10 May 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Gumzo kubwa kwa sasa kwenye Ligi ya Kikapu Marekani ni tuzo ya bora (NBA MVP) kuingia faianli bila kuwepo mchezaji raia wa nchi hiyo huku Nikola Jokic wa timu ya Denver Nuggets akitwaa tuzo hiyo mbele ya wapinzani wake Giannis Antetokounmpo na Joel Embiid.

Mastaa wote watatu walioingia fainali, walikata 'mzizi wa fitna' kwa kuwafunika wachezaji wote wa Marekani, ambao tangu tuzo hiyo ianze kutolewa msimu wa 1955-56 haijawahi kutokea tuzo kushindaniwa na wachezaji watatu wa mwisho ambao ni kutoka nje ya Marekani.

Hii imetokea msimu huu na sio kwa bahati mbaya bali kwa sababu ya ubora wa wachezaji wenyewe walioingia fainali hiyo ambao walistahili mbele ya wengine wote kwenye msimu mrefu wa ligi (Regular season) iliyochezwa mechi zote 82 kama kawaida, tofauti na misimu miwili iliyopita kuathiriwa na Covid-19.

Giannis Antetokounmpo wa timu ya Milwaukee Bucks ni raia wa Ugiriki na Nigeria, Nikola Jokic wa Denver Nuggets ni ni Mserbia na Joel Embiid wa Philadephia 76ers ni Mcameroon, wote waliupiga mwingi zaidi msimu wa ligi ulioisha mwezi April, huku kila mmoja akiwa na sifa ya kipekee iliyofanya aingie tatu bora ya kuwania tuzo ya MVP wa msimu.

Giannis msimu huu alicheza nje ya nafasi yake, kufuatia kuumia kwa mwenye nafasi yake Brook Lopez na 'akaupiga mwingi' pamoja na kuwa kwenye chati ya wachezaji waliofunga pointi nyingi zaidi nyuma ya Joel Embiid na LeBron James. Embiid kwa upande wake ndiye ameshinda tuzo ya ufungaji wa pointi kuliko wote kwa msimu akiwa na wastani wa pointi 30.6.

Upande wa Nikola Jokic yeye ameongoza kwa kuandikisha takwimu bora zaidi za muunganiko wa pointi, ribaundi, kuzuia na kupora mipira kwa wapinzani, huku pia akiwa mchezaji wa kwanza kwenye historia kwa kufunga pointi 2000, kudaka ribaundi 1000 na kuasisti mara 500. Joker pia ameshinda tuzo hiyo kwa kuongeza sifa ya kuongoza kufunga triple double mara 19, ndani ya msimu mmoja, ukiachana na kufunga double double mara 66, akimzidi Embiid aliyefanya hivyo mara 46. Vigezo hivi na vingine vimechangia wote watatu waingie fainali ya kuwania tuzo ya MVP kiasi cha kuzaa neno la tuzo inamstahili yeyote kati yao.

Sasa, tuzo hatimaye imempata mwenyewe! mshindi wa tuzo ya NBA MVP kwa msimu huu imekwenda kwa Nikola Jokic! Joker ameibeba kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuitwaa tuzo hiyo msimu uliopita akirudia kilichofanywa na Giannis Antetokounmpo ambaye aliibeba mara mbili mtawalia iliyopita kabla ya hii miwili ya Jokic.

Licha ya kuwepo na gumzo ambalo limeshtua tena, kwamba tuzo ilimstahili zaidi Joel Embiid lakini sifa kubwa ambayo imemuongezea sababu Joker kushinda ni ile ya kucheza msimu mzima bila kuwepo kwa mastaa wawili wa timu yake Nuggets ambao ni Jamal Murray na Michael Porter Jr, na kumfanya Jokic apambane kama jeshi la mtu mmoja na timu ikatoboa kucheza Playoffs.

Mjadala uliopo ni wa Nikola Jokic amestahili tuzo hii mbele ya Embiid na Giannis? Hii ikiwa ni kwa sababu wote walistahili kuibeba tuzo hiyo!

Chanzo: Mwanaspoti