Wenyeji Tanzania, timu ya Kurasini Heat itafungua dimba la michuano ya Ligi ya mpira wa kikapu Afrika (BAL) dhidi ya Brave Hearts ya Malawi kesho Ijumaa.
Kurasini Heat itacheza mchezo huo wa kundi E wa raundi ya awali saa 2 usiku kwenye uwanja wa ndani wa taifa, Dar es Salaam.
Timu nyingine za kundi hilo ni City Oilers ya Uganda na New Stars ya Burundi huku kundi lingine likiwa na timu za Ulinzi Warriors ya Kenya, Cobra Sport ya Sudan Kusini, Hawassa City ya Ethiopia na Ascut ya Madagascar.
Rais wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa amesema timu hizo zinashindana kusaka tiketi ya kufuzu kucheza hatua ya 16 bora ya Ligi hiyo.
Amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na timu shiriki kuanza kuwasili nchini tayari kwa mashindano hayo yatakayoanza saa 8 mchana kesho kabla ya mechi ya ufunguzi baadae usiku.
Kocha wa Kurasini Heat, Shendu Mwagala ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD) amesema maandalizi ya timu yao yamekmilika na wanaamini watafanya vizuri na kuingia kwenye hatua ya pili ya Ligi hiyo itakayochezwa nchini Rwanda.