NI mmoja ya wachezaji bora na kivutio kwenye mpira wa kikapu Tanzania kwa sasa kutokana na kiwango chache uwanjani ambacho kimekuwa kikiwavutia mashabiki wengi wa mchezo huo hapa nchini.
Namzungumzia Enerico Agustino, mchezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya ABC inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ).
Mchezaji huyu aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) baada ya kufunga pointi 263, pia aliibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Taifa (NBL) baada ya kufunga pointi 165.
Enerico pia aliibuka mchezaji bora wa mashindano ya NBL (MVP) kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha katika mashindano hayo yaliyofanyika mwezi uliopita mkoani Arusha huku akiipa ubingwa timu yake ya ABC.
Nyota huyo anasema Tanzania ina vipaji vingi vya mpira wa kipaku lakini miundombinu hasa viwanja, ligi kukosa wadhamini, ndio kikwazo kikubwa kinachoukwamisha mchezo huo ushindwe kusonga mbele.
Anasema wachezaji wengi wa hapa nchini wanacheza mchezo huo kama hobi tu kwa sababu wanaupenda lakini hauwanufaishi chochote kutokana na ligi mbalimbali kuchezwa bila udhamini hivyo timu kushindana bure tu bila kupata chochote.
Anasema wanahitaji wadhamini wengi kujitokeza kudhamini mashindano mbalimbali ili kuupa thamani mchezo huo.
“Lazima mchezaji anayecheza mchezo huu afaidike kwani kwa miaka ya karibuni mambo ni tofauti, wengi wanacheza lakini hawajui kikapu kinawanufaisha vipi tofauti na zamani watu walikuwa wanacheza mpira wa kikapu na unAwanufaisha.
“Nafikiri kuna kitu kinatakiwa kufanyika ili mchezo huu urudi juu kama zamani ikiwemo kutafuta wadhamini, vyama vya mchezo huu vinatakiwa kujipanga vizuri kwani wadhamini wengi wanaogopa kuingia kwa sababu hawajui hata mfumo wa ligi ukoje,” anasema Enerico na kuongeza
“Viongozi wa Shirikisho la kikapu, vyama wana kazi kubwa ya kufanya kuurejesha huu mchezo kwenye hadhi yake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Tunafurahi kuona CRDB inajitahidi sasa hivi kuingia na kudhamini mashindano mbalimbali na hiyo inatoa chachu kwa vijana wengi kupambana na kuja kwa wingi kucheza kwani kuna baadhi wanapata ofa za kusomeshwa kupitia mchezo huu hivyo tunahitaji kuona makampuni mengi zaidi yanajitokeza kwenye mpira wa kikapu kuja kudhamini kama ilivyo kwenye soka, ili wachezaji wengi wafurahie kucheza wakijua kuna kitu wananufaika nacho,” anasema Enrico.
Ameiomba Serikali kuutazama kwa jicho la tatu mchezo wa mpira wa kikapu kwani anaona imewekeza zaidi kwenye soka.
“Tunajua soka ni mchezo pendwa duniani na ndio maana hata serikali kwenye vikao vyao vingi wanaitaja sana soka lakini waangalie pia na michezo mingine ukiwemo huu wa kikapu nao unaweza kuiletea sifa nchi.
“Tunahitaji viwanja vingi vya ndani kwa ajili ya mchezo huu kwani tatizo la ukosefu wa viwanja ni kubwa hapa nchini na linahitajika kuangaliwa kwa upana na kupatiwa ufumbuzi ili kuzidi kuvumbua vipaji vingi kwenye mchezo huu,” anasema Enerico.
Akosa RBA, atwaaa NBL
Moja ya timu iliyokuwa kwenye kiwango bora kwenye RBA msimu huu ni ABC lakini ikajikuta ikishindwa kutwaa ubingwa mbele ya Savio licha ya kucheza michezo mitano ya fainali.
Jambo hilo lilimuumiza Enerico lakini mwisho akakubali matokeo lakini akaapa lazima watwae ubingwa wa mashindano ya Klabu bingwa Taifa (NBL).
Kweli buana, ABC wakapambana na kutwaa taji hilo la NBL na hivyo kutimiza malengo ya Enerico.
“Kukosa ubingwa wa RBA iliniuma, sio mimi peke yangu bali na wenzangu wote lakini mwishowe asiyekubali kushindwa sio mshindani.
“Tulipambana sana kwenye mechi zote tano za fainali na niseme kilichowasaidia Savio kutwaa ubingwa ni uwepo wa mchezaji wao, Hasheem Thabeet yaani yule ndio alikuwa kikwazo sana kwetu ila asingekuwepo tungewamaliza mapema tu hata mechi tano tusingefika,” anasema Enerico na kuongeza;
“Ujue Hasheem ni mchezaji jina na uzoefu sana na lile umbo lake alitupa shida sana kucheza nae.
“Tunashukuru baada ya kuukosa ubingwa wa RBA, tukatwaa ubingwa wa NBL katika mashindano yaliyokuwa magumu sana kwani hata mechi zote tulizoshinda tulipishana pointi chache sana na wapinzani wetu na hakuna mechi tuliyowazidi zaidi ya pointi 10,” anasema Enerico.
KIKAPU CHAMPA AJIRA
Kama ilivyo kauli mbiu ya siku zote kuwa michezo ni ajira basi Enerico alibahatika na kauli mbiu hiyo baada ya mpira wa kikapu kumpa ajira jeshini.
Alianza kucheza mchezo huo mwaka 2001 katika shule ya msingi ya Nyamalango iliyopo Mwanza na kufanya vizuri katika mashindano ya Umitashumta na kuuvutia uongozi wa shule ya Lord Barden iliyopo Bagamoyo inayomilikiwa na kanali mstaafu, Iddi Kipingu.
Shule hiyo ambayo inahusika na ukuzaji wa vipaji, ilimchukua Enerico na kumpa ufadhili wa masomo ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Wakati nasoma hapo Lord Barden pia nikawa nacheza mpira wa kikapu katika timu ya Savio na nilipomaliza shule nikajiunga na JKT na kuendelea kucheza hapo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.
“Mwaka 2017 nikaenda kozi ya kijeshi na niliporudi mwaka 2018 nikajiunga na ABC na nikaajiriwa mpaka leo,” anasema Enerico ambaye anadai alipenda kikapu kutokana na ushawishi wa kaka yake Frank Agustino ambaye alikuwa mchezaji mahiri wa mchezo huo.
WANAOMVUTIA
Licha ya kwamba amekuwa mfano kwa wachezaji chipukizi wanaomuangalia lakini hata yeye kuna mchezaji anayemvutia anapokuwa uwanjani ambaye anamtaja kuwa ni Alinani Andrew kutoka ABC.
“Alinani ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na yupo vizuri na anafanya vitu vikubwa uwanjani, nafurahi kucheza nae timu moja na kama akiendelea kucheza kwa ubora huo atafika mbali sana.
“Kwa upande wa wanawake kuna mchezaji wa Vija Queens anaitwa Noela yaani yule mchezaji vitu anavyofanya uwanjani na umbo lake hata haviendani, anaufanya mpira wa kikapu kuwa mchezo rahisi sana huwa napenda kumuangalia,” anasema Enerico.