Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

BARONGO: TBF mpya inakuja na ya kufurahisha

Barongo Pic MakamMwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, Rwehabura Barongo

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Desemba 30, 2021 Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) lilifanya uchaguzi mkuu wake ikiwa ni baada ya miaka minne kupita kama Katiba yao inavyowaongoza upande wa viongozi kukaa madarakani kwa kipindi hicho.

Uchaguzi huo ulifanyika jijini Dodoma na kumuweka madarakani Rais mpya Michael Kadebe akimwangusha Phares Magesa huku Makamu Mwenyekiti akichaguliwa Rwehabura Barongo aliyemshinda Mboka Mwamabusi wakati nafasi nyingine ya juu ya Katibu Mkuu ikienda kwa Mwenze Fiston Kabinda huku msaidizi wake ni Benson Nyasebwa.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Kamisheni ya Mipango na Maendeleo Fredrick Mtandu, Kamisheni ya Watoto na Mashule Bakari R Juma, Kamisheni ya Makocha Robert Mangerere, Kamisheni ya Ufundi na Mashindano Daniel Patrick, Kamisheni ya Fedha Leonard Haule na Kamisheni ya Waamuzi William Mziray.

Hivi sasa, mwezi mmoja tangu uongozi huo uingie madarakani, Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Makamu wa Rais wa shirikisho hilo Barongo anayeelezea mambo mbalimbali kwenye uongozi wao.

“Mwanzo nilikuwa nafanya tu kama hobi, baadaye niliona naweza kusaidia kwenye ngazi ya Taifa, huko nyuma nilikuwa nafikiria uongozi lakini kile kitendo cha kufanya kampeni kugombania kupiga kura kilikuwa kinanitoa kwenye mstari lakini ilifika wakati niliona kama kweli unaona vitu vinaenda kama usivyotarajia unaamua kuingia mwenyewe ili kuviendeleza,” anasema Barongo.

MABADILIKO TBF

“Ukiangalia hata jirani zetu tu hapa wanatufunga kila siku, kama unapata matokeo hayo ujue kuwa kuna kitu hakijaenda sawa, programu zetu haziko sawa kuanzia shuleni, mifumo kuanzia ngazi ya taifa hadi mikoani havijakaa sawa.

“Nilishangazwa kugundua kuwa hakuna chama cha mkoa ambacho kinalipa ada kwenye Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wakati Serikali ndio muhimili wetu mkuu, je, tutafanyaje kazi na Serikali kama hatutimizi yale tunayopaswa kuyatimiza?

“Kila chama kinapaswa kulipa ada ya Sh50,000 kwa mwaka ilipanda kutoka Sh20,000 na pia klabu zinapaswa kuwa zimesajiliwa kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zetu. Hivi vitu vinajulikana ila vilikuwa havitekelezwi kwa sababu ya mfumo uliokuwepo kuanzia Taifa hadi ngazi za huku chini.

“Niliona ni kitu kikubwa sana, kwa kuanzia hapo tunaweza kufanikiwa zaidi hata kwa wadhamini, mfano vyama havina hata akaunti za benki. Je, hata mdhamini akipatikana pesa ataingiza kwenye akaunti ipi ama ya mtu? Ukiangalia sera ya BMT zinaeleza kuwa kila chama lazima kifanyiwe ukaguzi wa hesabu sasa watakagua nini kama chama hakina akaunti ya benki na huwezi kukagua akaunti ya mtu.

“Kuna vitu tukiviweka sawa basi vitatusaidia hata kupata misaada zaidi FIBA maana kama nchi za wenzetu za jirani wamekamilisha na wanapata misaada, kuna changamoto ambazo tumezikuta na tumeanza kuzifanyia kazi ikiwemo kukutana na kujadili na wadau wetu ambao ni vyama vya mkoa,” anasema na kuongeza;

“Mchakato tayari unaendelea na sasa hivi tumefungua mawasiliano kwa njia ya barua pepe, pia kutakuwa na mikutano na barua, tunataka kujua mikoa ina timu ngapi, ma-RAC wao na wasajili wa vyama michezo mikoani.

“Ili kuendelea na programu ni lazima ujue mikoa ikoje na wakati mwingine tutalazimika kutumia hata wachezaji ambao wana uzoefu wa kuongoza, mfano Chama cha Mkoa wa Mara wenyewe tayari wana bajeti yao ya mwaka, wamemtafuta mlezi wa chama hivyo wanaonyesha mwanga.

“Kila mkoa utapaswa kuwa na mweka hazina ambaye amesomea kazi hiyo na ipo hata kwenye sera ya michezo ya BMT ili hata kama wakaguzi wanapoenda kufanya ukaguzi wajue wanashughulika na mtu wa aina gani,” anasema Barongo

KUJENGA OFISI

“Tumekubaliana na BMT kuwa tuwe tumepata ofisi yetu ndani ya miezi mitatu ili watu wanapokuja kupata huduma wajue kuwa wanapata wapi sio kama ilivyokuwa awali na tumeangalia sehemu kadhaa.

“Tutakuwa na Msemaji wa TBF ambaye atakuwa anahusika na vyombo vya habari moja kwa moja na tutamtangaza hivi karibuni, ili kuhakikisha vyombo vya habari vinapata taarifa za mara kwa mara, maana tunapaswa kuutangaza mchezo wetu na shirikisho letu ikiwemo kuwa na bidhaa zetu,” anasema Barongo ambaye amecheza mchezo huo kwa miaka 14 katika ligi ya NCAA Division akiwa Iduho State University, Marekani.

KUSHUKA / KUPANDA

“Tutatoa mwongozo kwa viongozi wa vyama vya mikoa ili kuishawishi jamii, kuanzia wazazi, shuleni ili waujue huo mchezo, ikiwemo serikali. Watoto waujue na kuupenda mchezo hasa shuleni kwa kuboresha mitaala na kuwafundisha watoto ili wawe wanaupenda huu mchezo kwa kufuata ngazi na hatua ya umri wa watoto,” anaeleza

VYANZO VYA MAPATO

“Kuna vyanzo karibu saba vya kutupatia pesa, kama udhamini, ada za wanachama, wachezaji kuwa kwenye data (wakisajiliwa watapaswa kulipia ada ya uhamisho pale ambapo mchezaji anahama kutoka timu moja kwenda nyingine hasa kwa timu za mkoa), kupitia mashindano ya ndani ambapo timu zinalipa ada ya ushiriki, tukiandaa mashindano ya kitaifa kuna pesa huwa tunapata.

“Ikumbukwe kuwa ada inayolipwa na vyama vya mikoa kule BMT pamoja na klabu ambazo pia zinalipa huko na kwenye vyama vya mikoa ila hata TBF nayo inalipa ada BMT,” anasema.

WALICHOKIKUTA OFISINI

“Hatuwezi kusema hatujakuta kitu, tumekuta mipira zaidi ya 20 ambayo tumekabidhiwa na vifaa vingine kwa kuanzia vinatosha kuleta maendeleo wakati tunapambana zaidi, ila sijui kama tulikuwa tunapata mipira ya kutosha ingawa FIBA nimezungumza nao na wametuambia tuandike mahitaji yetu ili kujua namna gani ya kutusaidia.

“Mipira tuliyoikuta inapaswa kugawiwa mikoani hata mmoja mmoja ili isiharibike halafu hapo baadaye kila kitu kitakaa sawa, maana mambo mazuri yanakuja.

MAJUKUMU

“Majukumu yangu makubwa ni kama mlezi, pia kuhakikisha naleta watu sahihi na kuweka mazingira bora ili kuleta maendeleo na hii ni kutokana na kwamba nimekaa na kucheza sana nje, lakini kila kiongozi kwenye kamisheni yake atafanya majukumu yake,” anasema Barongo.

“Tumeanza kuona ushindani mkubwa, ukiangalia ligi ya Dar es Salaam na Dodoma mwaka jana zilifanya vizuri, kama tumefanikiwa kwenye mchezo wa bao iweje tushindwe huku, kikubwa ni kuhamasisha na kuwafuatilia vijana.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz