Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Young Lunya: Hapa ni mwanzo mwisho na Sony Music Africa

Young Lunya Ll.jpeg Msanii wa Hip Hop, Young Lunya

Sun, 19 Jun 2022 Chanzo: Mwananchi

Msanii wa hip hop Bongo, Young Lunya amesema kusainiwa na Sony Music Africa ilikuwa kiu yake ya muda mrefu, kwani lengo ni kufikisha muziki wake kimataifa na tayari alishajiandaa kwa hatua hiyo.

Utakumbuka mwaka huu katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) Young Lunya alishinda tuzo mbili katika vipengele vya Msanii Bora wa Kiume wa hip hop na Wimbo Bora wa hip hop (Mbuzi).

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Sony Music Africa Juni 3, 2022, tayari Lunya yupo kwenye maandalizi ya albamu yake ya kwanza ambayo amewashirikisha Diamond Platnumz, Khaligraph Jones, Sho Madjozi na wengineo kibao wakichana ndani yake.

Akizungumza , Young Lunya amesema ngoma zake nyingi alizorekodi zinalenga soko la kimataifa, hivyo alikuwa anahitaji uongozi mzuri wenye uzoefu katika eneo hilo, hivyo kuwa chini ya Sony Music ni mafanikio makubwa kwake.

“Nimeipokea kwa furaha kwa sababu ndoto zangu zilikuwa ni kuja kufanya kazi na lebo kubwa ndio maana hata kazi zangu ambazo nilikuwa nazirekodi nilikuwa sizitoi hadi nije kupata uongozi ambao unakuwa unaelewa sana masuala ya muziki, kwa hiyo kwenda Sony Music ni kitu kikubwa sana,” amesema Lunya.

Huu ni usajili ya pili ulioufanya Seven Mosha tangu alipoteuliwa kuwa Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, staa wa kwanza kumsaini ni Ferregola kutoka DR Congo ambaye ameshaachia albamu yake, Dynastie yenye nyimbo 16.

Wimbo wa kwanza kwa Young Lunya kuuachia chini ya Sony Music unaitwa ‘Vitu Vingi’ ambao amesema unazungumzia mapenzi.

“Nimezungumzia kwamba kichwa kina vitu vingi ila haimaanishi kwamba sikupendi (mpenzi wake). Bado napambana kwa ajili yako, kwa hiyo ni wimbo wa kimapenzi lakini wa kitofauti kidogo”.

Akamilisha albamu

Young Lunya amesema albamu yake imeshakamilika kwa asilimia 90, na sasa vimebakia vitu vichache vya mwisho kama mixing, mastering na kupangiwa tarehe ya kutoka na Sony Music.

Amesema kufanya kazi na wasanii kama Diamond Platnumz, Khaligraph Jones na Sho Madjozi katika albamu hiyo ni hatua nyingine ya ukuaji wa muziki wake kibiashara na kimataifa.

“Ni hatua nzuri kufanya kazi na Diamond kwa sababu unakuwa unafanya kazi na msanii ambaye anajua biashara ya muziki, anajua nini kinafanyika, anataka hiyo kazi ije kuwa fedha, kwa hiyo ni kitu kikubwa sana,” amesema na kuongeza:

“Ukija Kenya, Khaligraph Jones ni msanii anayefanya vizuri huko, kufanya naye kazi itanisaidia kupenya Kenya kirahisi. Sho Madjozi wa Afrika Kusini ni msanii mkubwa kule kwao, ngoma zake zimefanya vizuri duniani, kwa hiyo ni kitu kizuri kufanya nao kazi.”

Hadi sasa kwa hapa Tanzania Lunya ameshafanya kolabo na wasanii kama Ommy Dimpoz, Nikki wa Pili, Mabantu, Country Boy, Maua Sama, Rosa Ree, Joh Makini, Mimi Mars, Haitham Kim, Moni Centrozone, Harmonize, Profesa Jay na wengineo.

Bado sana tuzo, Freestyle Session

Kushinda tena tuzo ya TMA 2022 ni miongoni mwa malengo aliyojiwekea Young Lunya kwa kile alichoeleza kushindwa kufanya hivyo, ni kuvuliwa ubingwa wake katika ulingo wa muziki, hasa hip hop.

“Napambana ili mwakani nisikose tuzo kwa sababu unajua kama nilishinda tuzo, mimi ndio ninayo, kwa hiyo kama mwakani mtu mwingine akichukua ina maana amenivua ubingwa, kwa hiyo inanibidi nifanye kazi na ninategemea nitachukua tuzo nyingine,” amesema Lunya.

Amesema licha ya kusainiwa Sony Music, bado ataendelea kufanya ‘Freestyle Session’ ambapo sasa yupo toleo la nne, kwani sio muda wote atakuwa anatoa ngoma.

“Ule ni mradi ambao nilianzisha kwa ajili ya watu wangu wanaopenda sana hip hop kwa sababu sio kipindi chote nitakuwa natoa nyimbo za Rap, kuna wakati nitatoa nyimbo ambazo zipo kwenye mfumo mwingine, kwa hiyo ni kitu ambacho kitaendelea kuwepo katika maisha yangu yote,” amesema Lunya.

Freestyle Session za Lunya zimekuwa vikivutia mamilioni ya watazamaji kwenye mtandaoni wa YouTube na kuwa msanii pekee wa hip hop Bongo kupata mafanikio hayo na hata kufanya jambo kama hilo.

OMG na kujiita Mbuzi

Ikumbukwe Lunya alikuwa kwenye kundi la OMG liloundwa na wasanii watatu, wengine ni Salmin Swaggz na ConBoi, walitamba na ngoma kama Fit, Wanangu na Wanao, Staki, Swing, Uongo na Umbea na Paradiso. Lunya amesema bado anaikumbuka familia hiyo kwani waliishi vizuri.

Katika hatua nyingine, Lunya amesema kujita Mbuzi, yaani (G.O.A.T) akimaanisha the Greatest of All Time, ni kutokana na kuutumikia muziki kwa miaka 11.

Ikumbukwe mkali mwingine wa hip hop Bongo, Fid Q anajiita Mzee Mbuzi, wasanii wengine waliojipa majina ya wanyama kwa muktadha wa kudhihirisha ukali wao ni Diamond Platnumz (Simba), Harmonize (Tembo), Rayvannny (Chui), Country Boy (Fisi), Dudu Baya (Mamba), Afande Sele (Simba) na wengineo.

Chanzo: Mwananchi