Wasanii wa muziki kutokea Uingereza, Marekani, Puerto Rico na Korea Kusini ndio pekee wameingia 10 bora katika orodha ya wasanii na matamasha 25 yaliyoingiza fedha nyingi kwa mwaka 2022 unaoelekea kuisha.
Eltno John wa Uingereza ndiye wa mwisho akiwa nafasi ya 25, huyu alifanya shoo mbili katika uwanja wa Gillette huko Foxborough na kupata mashabiki 96,039 na kuingiza kitita cha fedha Dola16.6 milioni, wastani wa Sh38.7 bilioni.
Katika orodha hiyo iliyotolewa na Jarida la Billboard ikiwa imekusanya data tangu Novemba 1, 2021 hadi Oktoba 31, 2022 kama ilivyo taratibu zao, hakuna msanii wa Afrika ambaye jina lake limechomoza.
Hawa ni wasanii na matamasha katika 10 bora yaliyopiga mkwanja mrefu mwaka 2022 pamoja na historia na rekodi zao katika muziki;
1. Harry Styles – Sh147.0 bilioni
Amefanya shoo 15 chini ya Live Nation (Promota) katika ukumbi wa Madison Square Garden, New York ambapo viingilio vilikuwa kati ya Dola119.50 hadi Dola39.50 (Sh278,000 / Sh92,000), hivyo kwa ujumla katika shoo hizo 15 zilizohudhuriwa na watu 276,852, ameingiza Dola63.1 milioni, wastani wa Sh147.0 bilioni.
Harry Styles ni miongoni wa wasanii wa Uingezra waliouza zaidi duniani, ameshinda tuzo za Brit, Grammy, Ivor Novello na AMA’s, albamu yake ya pili, Fine Line (2019) ilishika nafasi za juu chati za Billboard 200 na miongoni mwa albamu 500 bora kwa muda wote katika orodha ya Rolling Stone.
2. Ed Sheeran – Sh86.8 bilioni
Huyu chini ya FKP Scorpio na Kilimanjaro Live amefanya shoo 5 zilizoingiza watu 420,269 katika uwanja wa Wembley, London, viingilio vilikuwa ni Dola97.93 hadi Dola61.20 (Sh228,000 / Sh142,000), hivyo kwa ujumla akaingiza Dola37.2 milioni, wastani wa Sh86.8 bilioni.
Naye anatokea Uingereza, wimbo wake ‘Thinking Out Loud’ kutoka katika albamu yake ya pili ‘X’, kwa mara ya kwanza ulimuwezesha kushinda tuzo mbili za Grammy 2016 kama Wimbo Bora wa Mwaka na Mtumbuizaji Bora wa Pop.
3. BTS – Sh83.6 bilioni
Watu 199,697 walihudhuria katika shoo zao nne chini ya HYBE katika uwanja wa Allegiant, Las Vegas ambapo viingilio vilikuwa ni Dola275 hadi Dola60 (Sh641,00 / Sh140,000), hivyo wakajipatia Dola35.9 milioni, wastani wa Sh83.6 bilioni.
BTS au Bangtan Boys, ni kundi kutokea Korea Kusini, lilianzishwa mwaka 2010, mwaka 2013 wakasaini Big Hit Entertainment, kupitia video ya wimbo wao, Butter (2021) wanashikilia rekodi ya dunia kwa kupata watazamaji milioni 108.2 YouTube ndani ya saa 24!.
4. Outside Lands And Music Festival – Sh79.1 bilioni
Katika ukumbi wa Golden Gate Park, San Fransisco, California wamefanya shoo tatu chini ya Another Planet Entertainment na kupata mashabiki 222,518 ambao walilipa viingilio Dola395 hadi Dola 175 (Sh921,000 / Sh408,000), jumla wakachukua Dola33.9 milioni, wastani wa Sh79.1 bilioni.
Hili ni tamasha kubwa zaidi la muziki ambalo hufanika kila mwaka huko California, Marekani, watu zaidi ya 200,000 hushiriki, mwaka 2019 liliandika rekodi kama tamasha liloingiza fedha nyingi zaidi duniani ikiwa ni Dola30 milioni, wastani wa Sh70.0 bilioni.
5. BTS – Sh77.7 bilioni
Kwa mara nyingine tena chini HYBE, BTS walifanya shoo nne ukumbi wa SoFi, Inglewood, California na kupata wahudhuriaji 213,751 ambao walilipa mlangoni Dola155.87 (Sh363,000), hivyo kuwapatia Dola33.3 milioni, wastani wa Sh77.7 bilioni.
Ikumbukwe mwaka 2020 BTS waliandika rekodi ya kuwa wasanii wa kwanza kutoka Korea Kusini kushika nafasi ya kwanza chati Billboard Hot 100 na Billboard Global 200, huku wimbo wao ‘Dynamite’ ukichaguliwa kuwania Grammy.
6. Bad Bunny – Sh72.3 bilioni
Watu 99,816 walihudhuria katika show zake mbili chini ya Gardenas Marketing Network na Live Nation katika ukumbi wa SoFi, Inglewood, California ambapo viingilio vilikuwa ni Dola1,000 na Dola 59.50 (Sh2.3 milioni / Sh138,000), jumla alichukua Dola31.0 milioni, wastani wa Sh72.3 bilioni.
Huyu ni Rapa kutoka visiwa vya Puerto Rico, anafanya ‘trap’ ya Kilatini pamoja na reggaeton, mwaka 2016 alivuma sana na wimbo wake ‘Diles’ hadi kupata dili la kusaini Lebo ya Hear This Music.
7. Cold Play – Sh65.3 bilioni
Chini ya Live Nation walifanya show nne katika uwanja wa Stade de France, Paris zilizopata mashabiki 318,331, viingilio ni Dola127.58 na Dola25.52 (Sh297,000 / Sh59,000), hivyo wakapata Dola28.0 milioni, wastani wa Sh65.3 bilioni.
Cold Play ni Band ya muziki kutokea Uingereza iliyoanzishwa mwaka 1997 baada ya kutana katika Chuo Kikuu cha London, mwanzo walijiita ‘Starfish’ kabla ya Cold Play. Albamu yao ya kwanza, Parachutes (2000) ilishinda tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka Uingereza pamoja na Grammy.
8. Lollapalooza Brasil – Sh54.1 bilioni
Katika shoo zao tatu ndani ya Autogrom de Interlagos huko Sao Paulo walipata watu 267,446, viingilio vilikuwa Dolla414 na Dola 44.13 (Sh966,000 / Sh102,000) huku TFF-TimeFor Fun akiwa ndiye Promota, kwa jumla walichukua Dola23. 2 milioni, wastani wa Sh54.1 bilioni.
Hili ni tamasha la muziki ambalo hufanyika kila mwaka nchini Brazil katika jiji la Sao Paulo tangu mwaka 2012, wasanii kama Pharrell Williams na Black Keys wamewahi kitumbuiza, huku mwaka 2023, Lil Nas X na Drake tayari wametangazwa watakuwepo.
9. Bad Bunny – Sh53.0 bilioni
Naye kwa mara nyingine tena ndani ya 10 bora, watu 84,865 walihudhuria show zake mbili chini ya Gardenas Marketing Network na Live Nation katika ukumbi wa Yankee, Bronx, New York ambapo viingilio vilikuwa ni Dola1,000 na Dola 59.50 (Sh2.3 milioni / Sh138,000), hivyo akapata Dola22.75 milioni, wastani wa Sh53.0 bilioni.
Ikumbukwe Bad Bunny alipata umaarufu zaidi mwaka 2018 baada ya kusikika kwenye wimbo wa Cardi B ‘I Like It’, pamoja na wimbo wake ‘Mia’ akimshirikisha Drake. Albamu yake ya kwanza ‘X 100pre’ chini ya Rimas Entertaiment ilishika nafasi ya 11 chati za Billboard 200.
10. Queen + Adam Lambert – Sh53.0 bilioni
Walifanya show 10 katika ukumbi wa 02 Arena, London chini ya Phil Mclntyre Entertainment na kupata watu 174,485, viingilio vilikuwa ni Dola1,102 na Dola56.18 (Sh2.5 milioni / Sh130,000), hivyo jumla wakachukua Dola22.74 milioni, wastani wa Sh53.0 bilioni.
Queen + Adam Lambert (Q+ AL au QAL), ni muunganiko wa wasanii, Brian May na Roger Taylor wa Band ya Uingereza, Queen na Mwimbaji wa Marekani, Adam Lambert. Huu ni ushirikiano wa muda mrefu zaidi wa Band hiyo tangu kumalizika kwa mradi wa Queen + Paul Rodgers mwaka 2009.