Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigumu kumuelewa Jux kama dunia imekutenga

46989 Pic+jux

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni ‘bishoo’. Yes kama usafi ni ubishoo basi dogo ni ‘bishoo’ kinoma. Septemba 1, mwaka huu anatimiza miaka 30. Nimedata. Mwambie. Uzuri Wako. Nitasubiri. Sisikii. Juu na Utaniua. Yote hayo ni majina ya ngoma zake zilizotamba. Na zaidi anammiliki mtoto mzuri Vanessa Mdee. Mungu ampe nini zaidi Juma Mussa ‘Jux’?

David Robert Beckham, soka lake lilikuwa la kawaida mbele ya masela waliomzunguka. Toka Manchester United ya Scholes na Cantona mpaka Real Madrid mbele ya Zidane na Ronaldo De Lima. Lakini ukubwa wa jina lake akawa kama Lowassa yule wa ndani ya CCM kabla ya 2015. Alikuwa taasisi ndani ya taasisi.

Man United iliposafiri kwenda Mashariki ya mbali kwenye maandalizi ya ligi (Pre season) timu ilipokewa kwa uzito uleule sawa na Beckham kama Beckham. Utawaambia nini Waingereza na Becks wao? Wakaamua kumfananisha na Yesu. Akatajirika kwa soka na pesa za nje ya soka kupitia umaarufu wa jina lake kimatangazo.

Kuna watu wana vipaji vya kupendwa. Wema Sepetu ni miongoni mwao. Hakuwa miss pekee aliyefanya maajabu kwenye shindano hilo kwani mafanikio ya Nancy Sumary Miss World 2005 yalikuwa makubwa zaidi. Lakini jina lake halimo kwenye vichwa vya vijana wengi. Wanamjua zaidi Wema Sepetu kuliko yeye.

Achana na Wema ambaye hivi sasa jina lake linafubaa. Kama uliwahi kumshuhudia Nature kwenye utawala wake wa Bongo Fleva utaelewa maana ya kupendwa ni kipaji. Kulikuwa na vipaji vingi ambavyo yeye hakuenea hata kiganjani mwao, lakini shoo kufanyika Dar bila Kibra Matata, shughuli isingekuwa shughuli.

Wakati jua la utawala wake likielekea Magharibi. Pale Leaders Club alikuja mwanadada Lil Kim toka Marekani. Bahati mbaya alikutana na kizazi kisichomuelewa. Akaumiza mbavu na mishipa ya shingo kulazimisha waende naye sawa. Wakawa hawamuelewi. Fasta Juma akainuliwa, Kibra, Sir mwenye Nature yake.

Mwili mdogo, sura ya Kiswahili. Mavazi ya uchumi wa kawaida. Swaga za Temeke, tabasamu lenye hisia za kisela, mchizi toka kiumeni pande za Kurasini. Alipojitokeza umati uliotulia kama unasikiliza matangazo ya vifo, ulilipuka na kumuacha kinywa wazi Lil Kim. Kabla ya kuungana naye kama mgambo wanaoruka na kukanyagana.

Mwisho wa shoo Kim aliishia kumuambukiza mtoto wa Kiswahili uturi wa marashi toka Campton, kwa kumbatio hatari. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kumshukuru kuokoa shoo yake. Kwa miaka hii ya ‘kiki’ za ‘insta’ tungesikia Kim ana mimba ya Nature. Lakini yeye kimya kimya alirudi Temeke na kuberi zake. Marehemu Amina Chifupa hakuwa mtangazaji wa ajabu, lakini siyo tu alikuwa maarufu, pia alipendwa zaidi. Umaarufu wake ukawa juu kuliko kituo cha redio aliyofanyia kazi (Clouds Fm). Alipata umaarufu kabla redio haijasikika Kiluvya, Bunju na Chanika achilia mbali Kinyerezi. Alikuwa staa anayeuza udaku kila siku.

Maana yake ni kwamba unaweza kuwa na kipaji kikubwa lakini ukakosa kipaji cha kupendwa na watu. Wakaishia kusema huyu kaka/dada anaimba sana au anaigiza sana - basi, lakini mwingine asiwe na uwezo wowote wa kuigiza au kuimba. Lakini akipita sehemu mpaka nyasi zinaduwaa.

Unamjua Rama Dee? Kama humfahamu ni mwanamuziki ambaye yeye na muziki wake hawajatendeana haki. Rama anaudai muziki na muziki unamdai. Jamaa anajua kiasi kwamba ukimuweka yeye na Jux, unaweza kufunguliwa mashtaka.

Wote wanafanya R&B, lakini huhitaji barua ya Basata kuambiwa kuwa Rama ni bora zaidi. Lakini Wabongo wengi wanamfahamu Juma Jux hivi sasa. Kama ilivyo kwa David Beckham kujiweka kwa Posh na kupata ustaa zaidi, naye Jux jina lilipaa zaidi baada ya kujiweka kwa mtoto mzuri Vanessa Mdee. Ukikutana na msichana yeyote hivi sasa ukamuuliza juu ya uwezo wa Jux na Rayvanny asilimia kubwa utaambiwa Rayvanny ni mkali sana kwenye kuimba. Kabla haujaendelea kuuliza kingine utapewa jibu ambalo hujauliza kuwa, lakini Jux anajua kuvaa. Jamaa hapo ndipo aliposhikilia kama nguzo yake.

Jux ni ‘bishoo’ mpaka ‘ubishoo’ wenyewe unamuonea aibu kukaa naye karibu. Hapo ndipo kwenye msingi wa muziki wa Jux. Kulipuka vitu mwilini. Kupigilia pamba na kujihusudu kwa usafi uliopita viwango vya TBS na TFDA. Kuna wakati mtu unapata shida kujua Wasafi kwa nini wajiite Wasafi mbele ya msafi Jux?

Kina Diamond watamfunika kwa kubadili totoz za mataifa mbalimbali. Watamfunika kwa shoo na kutoa nyimbo nyingi. Watarukaruka kwenye mambo mengine, lakini kwenye suala la kutupia matambara mwilini anawaacha maili nyingi sana. Diamond atavaa vazi la bei ghali zaidi, lakini siyo kulipuka pamba kama Jux.

Hapo ndipo alipowakamata totoz. Muziki biashara yake utaiona tamu ukiwanasa wasichana, ndiyo walaji wa muziki duniani. Kuwakamata ni mafanikio makubwa kimuziki. Watadondosha chozi ukiwa jukwaani. Watakusikiliza nyumbani, barabarani mpaka ofisini. Upendo huu wa Agape huwezi kuupata kwa masela.

Kiba atamfunika Jux kwa sauti. Utunzi na ukubwa wa jina na mbavu zake, lakini kwenye suala la kutupia anaachwa kilomita nyingi. Na warembo huvutiwa na vitu vingi, lakini suala la kunyuka vitu vilivyonyooka mwilini huwavuruga akili. Muonekano kwa totoz ni zaidi ya vumbi la Congo. Uliza watoto wa mjini.

Jux hana muziki wa kutisha. Na kumekuwa na maneno mitaani kuwa anaimba ila siyo kwa kiwango cha juu. Ndiyo hata yeye naamini anafahamu kuwa Mungu hamkubariki uwezo wa Q Chilla au Ben Pol, lakini ana kitu cha ziada ambacho pia ni sehemu ya muziki. Muonekano ni sehemu ya muziki. Hili liliwashinda kina Twenty Percent.

Uvaaji wa kisela ilikuwa silaha wakati ule muziki wakiimbiwa masela zaidi. Ndipo watu sampuli ya Nature walishika soko. Lakini hizi ni nyakati za kina Jux, dunia ya kujilipua kwa pamba na muonekano. Hapa nd’o kwenye eneo tengefu kwa Jux. Kafanikiwa sana kwani anaongelewa kwa uvaaji kuliko uimbaji. Kabla ya kipaji chake angalia aina ya mashabiki wake. Na anawanasa kwa lipi? Wengi ni mademu na sumu yake kwao ni upigaji wa pamba. Na zaidi dawa ya demu ni demu. Vanessa kukaa kando ya Jux ni silaha nyingine. Mademu huvutiwa zaidi na msela mwenye demu mkali. Bila kuyaelewa haya, dunia itakuacha hapo hapo.



Chanzo: mwananchi.co.tz