Baada ya ukimya wa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, hatimaye mwimbaji wa Bongofleva, Aslay amewapa mashabiki wake muziki wake kile walichokosa kwa muda mrefu kwa kuachia ngoma mbili, ‘Mozzah’ na ‘Follow Me’ akimshirkisha Harmonize.
Hata hivyo, ujio huu ni darasa kwa wasanii na mashabiki kuhusu starehe, matumizi ya fedha, nidhamu ya kazi, umilivu na kukubali kuanza upya. Aslay alikuwa miongoni mwa wasanii wanne waliounda kundi la Yamoto Band lilovunjika rasmi mwishoni mwa mwaka 2016, wengine ni Mbosso, Enock Bella na Beka Flavour.
Baada ya kuachana na Yamoto Band, Aslay aliweza kutoa nyimbo 15 ndani ya miezi 11 (Aprili 10, 2017 hadi Februari 22, 2018) na kupata mapokezi makubwa.
Ujio wake huu mpya, ni baada ya kusaini kufanya kazi na Menejimenti ya RockStar Africa na Lebo ya Sony Music Entertainment Africa, akiwa ameungana na Ommy Dimpoz, Abigail Chams na Young Lunya kwa hapa Tanzania.
Aslay alikuwa kimya tangu alipoachia wimbo wake ‘Nashangaa’ hapo Januari 2021, na tangu kabla ya hapo hakuwa na wakati mzuri wa kuachia ngoma kama ambavyo mashabiki wake walikuwa wamemzoea.
“Nilidanganywa sana, niliibiwa sana, karibia nipoteze maisha yangu kwa msongo wa mawazo kwa kunywa pombe, na msongo wa kumkumbuka mama yangu, lakini yote ni ustaa na nilichagua mwenyewe maisha ya kuwa staa” Aslay akieleza sababu za ukimya wake.
“Sasa hivi nimekua, akili yangu imekua na nina uzoefu wa yote niliyopitia, sasa ni kufanya kazi na kuangalia maisha mengine mapya” anasema Aslay katika dokumentari yake, Mimi ni Bongo Fleva.
Aslay anasema kutokana na kuanza muziki akiwa na umri mdogo, alipata mafanikio akiwa na umri mdogo pia, akiwa na miaka 20 tayari alijua milioni 1 hadi 3 ipoje, na hata alipoanza kufanya muziki kama solo fedha alipata nyingi ndipo mambo yakamzidia!.
“Kwa hiyo mafanikio yalinichanganya, siwezi kuongopa, mafanikio yalinipeleka puta kiasi kwamba yalinitoa kwenye mchezo kwa sababu nilipata marafiki wapya na washauri tofauti tofauti” anasema.
“Starehe zilikuwa ni nyingi kwa sababu nilikuwa naweza kufanya kitu chochote kwa sababu fedha nilikuwa nazo, kwa hiyo kujiamulia kufanya kitu nilikuwa na uwezo huo. Baadaye nikaingia kwenye pombe, wanawake hadi sasa nikawa nasahau kilichonifanya hadi vitu vyote vikanifuata” anasema Aslay.
Anasema wakati yupo katika kilele cha mafanikio kila mtu alikuwa anataka kufanya kazi naye, na kikubwa zaidi Lebo kubwa tatu zilimfuata ili kufanya naye kazi ila alikataa kutoka na aina ya mikataba waliyompa.
“Lebo ya kwanza ilikuja, walivyonielezea sikupendezewa na mikataba yao, jinsi wanavyotaka, kwa sababu mimi ni mtu ambaye napenda sana kujiamini, yaani mtu fulani wa kujitoa, kwa hiyo sipendi sana kubanwa kwenye kazi zangu, hivyo nilishindwa kusaini” amesema Aslay.
Kukutana kwake na Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment Africa, Christine “Seven” Mosha, anasema kumemfanya ajue zaidi biashara ya muziki na umuhimu wa Rekodi Lebo na Menejimenti, ndipo akaamua kujiunga upande huo.
“Kwa hiyo Madam Seven ni mtu ambaye amenishauri, amenielekeza, pia amenipa hongera kuvumilia vitu vingi. Naweza kusema yumo ndani ya ndoto zangu kwenye maisha yangu, ni mtu ambaye amenitoa sehemu moja kwenda nyingine” anasema.
Anasema kusaini Sony Music Africa, kwanza ilikuwa shauku yake ila ilikuwa inaenda na kupotea sababu ashaumwa na nyoka!.
“Nishadhulumiwa, nishaongopewa halafu nikisikia hizi Lebo watu wanaibiwa ilikuwa inanichanganya sana nisije kuingia sehemu ambazo wenzangu waliingia wakafeli. Kwa hiyo mara nyingi nilikuwa namsumbua Madam Seven ili anieleweshe, kwa hiyo mimi kusaini Sony Music nimefurahi sana kwa sababu naona ndoto zangu zinapoelekea,” anasema Aslay.
Tukirudi nyuma, Aslay amesema kusimamiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi, Clouds Media Group, Marehemu Ruge Mutahaba haikuwa kwa lengo la kushindana na msanii yeyote.
Anasema alifanya kazi na Ruge kama alivyo kwa wasanii wengine Tanzania, hivyo mashabiki na wanaomfuatilia kila siku waelewe hajawahi kushindana na mtu kwenye muziki wake, na kwanza hawezi kushindana na kitu ambacho anakiweza!.
“Nilishasema nilianza mwenyewe, nimepigana na nimeangaika mwenyewe kwenye muziki wangu, siwezi kushindana na hata kipindi nafanya kazi na Ruge, hakunichukua ili kushindana na mtu, nilifanya naye kazi kama wasanii wengine” anasema.
“Alinichukua kwa vile ninaandika vizuri, naimba vizuri, ndio kitu alichopenda, pia alinichukua kama msaada, kuna vitu vingine sitaki kuongea, kwa sababu nilipokuwa naenda pale THT kuonana na Ruge, pia nilipata hata bahati ya kumsaidia Nandy, nilikuwa sitaki kuongelea hili suala lakini ni kitu kipo wazi watu wanajua” amesema Aslay.
Wimbo wake mpya ‘Mozzah’ ni kwa ajili ya kumuenzi Marehemu mama yake na anataka kila shabiki yake kuungana naye katika kumpenda.
“Dunia nzima iungane na mimi kumpenda mama yangu kwa mtindo ambao ninaujua mimi, nao ni muziki tu kwa sababu unatufanya tuburudike, tufurahi, pia tukumbuke mema ya mama yangu na utatufanya tusahau mabaya yote ambayo nimepitia. Naamini hakuna kitu kingine zaidi ya muziki” anasema Aslay.
Na kitendo cha Aslay kumshirikisha Harmonize katika ngoma yake ‘Follow Me’, kumemfanya Konde Boy kufikisha jumla ya nyimbo 12 alizoshirikishwa mwaka huu pekee, huku akiwa ndiye msanii aliyeshirikishwa zaidi.
Utakumbuka Harmonize amesikika kwenye ngoma kama; Closer (Abigail Chams), My Baby (Roberto), Bad Man (Tundaman), Utamu Remix (Mabantu), Ni Wewe (Killy), Naogopa (Marioo), Kioo (Anjella), Furaha Remix (Iyanii), Addiction (Ibraah), Champion Remix (Kontawa), Konkodi (Cheed) na Follow Me (Aslay).