Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sura tatu uteuzi wa Steve Shirikisho la Muziki

Stevenpic Steve Nyerere

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: Mwananchi

Kwa wiki ya pili sasa, habari iliyoteka vichwa vya habari ni ya msanii wa vichekesho, Steve Mengele, maarufu Steve Nyerere, kuteuliwa kuwa msemaji wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT).

Uteuzi huo wa Steve ulitangazwa Machi 16 mwaka huu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa juu wa shirikisho hilo, akiwemo Rais wake, Ado Novemba, Makamu wa Rais, Mzee Yusufu, Katibu Mkuu Farid Kubanda ‘Fid Q’, Katibu Uenezi, Siza Mazongera na mlezi wa shirikisho, Asha Baraka.

Tangu Steve alipotangazwa umeibuka mjadala ulioanzia kwenye mitandao ya kijamii kwa wasanii na wadau mbalimbali kupinga maamuzi hayo.

Baadhi ya wasanii, hususan wa muziki wakiwemo wakubwa, walitumia kurasa zao kulaani hatua hiyo.

Novemba alitetea uteuzi huo kwa madai kuwa ni kupata nguli wa kusemea shirikisho, mwenye kujua muziki, mwenye watu, mwenye heshima ndani na nje ya nchi.

Kama haitoshi, Novemba alisema Steve ni msaada kwa wasanii, kwani hivi majuzi kuna msanii alifiwa akapeleka magari ya kubeba abiria aina ya coaster matano na kuwalipa posho waliokwenda msibani, pia wanapokuwa maeneo mbalimbali amekuwa mlipaji bili mzuri wa vitu ambavyo wasanii wamekuwa wakivitumia bila kuhoji.

Kwa aliyoyasema yote haya, ukiangalia kwa undani sakata hili limejaa mambo makubwa matatu, yakiwemo maslahi, siasa na ubongofleva.

Hata hivyo, kutokana na mgogoro uliopo Steve Nyerere ametangaza kujiuzulunafasi hiyo, siku moja baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kumsimamisha kuongoza shirikisho hilo. Maslahi

Suala la maslahi katika sakata hili limetawala. Novemba alidai kuwa Steve amekuwa akishirikiana na baadhi ya wasanii katika mambo mbalimbali yakiwamo ya furaha na huzuni, huku akijitolea kwa hali na mali. Hii inaweza kuwa sababu ya kuteuliwa kwake kwa sababu yupo karibu na baadhi ya wasanii.

Pili, baadhi ya wajumbe kuwa katika muziki wa taarabu na dansi ambao unaonekana kutowanufaisha na Steve alijinasibu kuuinua, pia kumechangia uteuzi wake.

“Ndani ya uongozi wangu siwezi kukubali kiingilio kiwe bia kwenye shoo za taarabu na dansi, nitarudisha mabonanza likiwamo la Leaders, pia nitasimamia wasanii kwenda kwenye matamasha nje bila kujuana bali watakwenda ambao ni wanachama wa shirikisho,” alisema Steve mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Siasa

Ukiacha maslahi, sakata hilo pia limevaa sura ya siasa, kwani tukianza na Rais wa Shirikisho Ado Novemba, alisema wanaopinga kuwepo kwa Steve Nyerere wengi ni wanaharakati na wapinzani ambao wamekuwa wakiikosoa mara kwa mara Serikali.

Ukiacha Ado, Steve katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa anawajibu waliompinga, aligusia mara kwa mara ubunge wa Mwana FA kwa kwenda mbali na kusema ni ubunge wa vikaratasi huku akimtaka asijisahau.

Akilitolea ufafanuzi hilo, MwanaFA anasema katiba ya shirikisho, Steve hana sifa ya kupewa nafasi hiyo, ikiwemo kutokuwa mwanamuziki.

“Jingine katiba inasema Katibu wa Mahusiano wa kitaifa na kimataifa, atagombea nafasi hiyo ambapo hili halijafanyika, kuwa na uzoefu wa mahusiano ya kimataifa, kuliunganisha shirikisho na vyama vya kimataifa, bodi ya shirikisho na atakuwa msemaji na muandaaji wa matukio mbalimbali, mambo ambayo Steve hakidhi sifa hizo,” alisema MwanaFA.

Ubongofleva

Wakati kikao cha kupokea maoni kilivyokuwa kinaendelea, baadhi ya wasanii wa dansi na taarabu ambao walionekana kuwa wachache, walilalama kuwa Bongofleva wameongea sana, ni muda sasa wa kuwaacha nao watoe maoni yao.

Kauli hiyo ilitolewa na mwimbaji wa Muziki wa dansi kutoka bendi ya Kale Musica, Andrea Mwapashi, ambaye alikutana na zomeazomea kutoka upande wa pili kwa kumjibu kuwa hakuna aliyewazuia kuongea.

Mwimbaji taarabu, Abdul Misambano anasema endapo jambo la kumkataa Steve lingeibuliwa na wasanii wa dansi, taarabu au muziki mwingine, kusingekuwepo na kelele hizo.

“Sisi wasanii wa dansi na taarabu tunamkubali Steve Nyerere kutokana na ushawishi kwenye jamii, BongoFleva kama hawamtaki watafute msemaji wao,” alisema Misambano.

Novemba alisema tatizo ni wasanii wa Bongo fleva hususan hiphop kuwa wabinafsi na kujiona wao wana haki ya kuwasemea wengine, jambo ambalo sio zuri.

Kauli hiyo ilipingwa na mwongoza video wa siku nyingi, Adam Juma.

“Hakuna namna ya kuwakwepa wasanii wa Bongo fleva kwa sababu ndio muziki unaotamba kwa sasa na umetoa ajira nyingi ndio maana wanapoongea jambo lao huwa kubwa.

“Viongozi wanapaswa kuelewa Bongofleva ni maisha, ajira na ustawi wa vijana, sio wa kuchezewa chezewa kwa kuwa kuna waliokuwa watoto ndani ya tasnia hiyo mpaka sasa ni mama na baba wa familia na wengine ni viongozi wa wananchi kwa sasa,” alisema.

Kuhusu uteuzi wa Steve, alisema hana analolijua, ila anachojua wasanii wa Bongofleva wanastahili kusikilizwa badala ya kuchukuliwa kama wahuni.

Chanzo: Mwananchi