Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIMULIZI ZA MUZIKI: Leo nimeukumbuka wimbo Sogea Karibu utunzi wa Belesa Kakere

60822 Pic+kitime

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sogea karibu nikueleze, usije shangaa imekuwaje

Upate fahamu na kuelewa, kuwa ndoa yetu sasa imevunjika -Chake

Nilikupeleka kwa wakwe zako, ukaonane na ndugu zangu

Hata mama yangu alifurahi sana na ndugu zangu walikupenda sana

Mapatano yetu dada ni kuoana kama tukichunga heshima yetu...

Hayo ni maneno ya wimbo uliotungwa na Salehe Belesa Kakere wakati huo akiwa Juwata Jazz Band. Alikuwa mtunzi na muimbaji mahiri aliyepata sifa katika bendi zote alizowahi kupitia na kurekodi, zikiwamo Biashara Jazz Band, Bima Jazz Band, Dar es Salaam International Orchestra, Juwata Jazz Band.

Pia Soma

Wimbo huu huu Sogea Karibu, ulioshirikisha wanamuziki wazuri wakati huo, umeendelea kupendwa miaka zaidi ya 40 toka utungwe. Kati ya washiriki wa wimbo huo, ambao wengi wao sasa marehemu ni Kassim Mponda aliyepiga gitaa la solo, marehemu Hondohondo gitaa la bezi, marehemu Siddy Morris aliyepiga drums, Dullah alipiga gitaa la rhythm, Waziri Ally ‘Kissinger’ kwenye kinanda huku waimbaji wakiwa Belesa Kakere na Hassan Bitchuka. Wimbo wote ni matukio ya kweli. Belesa alikuwa na mpenzi aliyeitwa Chake, ambaye walikutana wakati akiwa JUWATA Jazz Band jijini Dar es Salaam. Dada yake Belesa naye alimpenda sana wifi yake akaamua kumchukua na kumpeleka Tanga walikokuwa wakiishi wazazi wa Belesa ili amtambulishe.

Binti alipokewa vizuri huku na wazazi wa Belesa pia wakamfurahia. Lakini baada ya muda mfupi uhusiano wa binti huyo na wenyeji wake ukabadilika, akakorofishana na wakwe na mashemeji zake wote.

Hatimaye akarudi Dar es Salaam kwa wazazi wake. Kutokana na hali ya mawasiliano siku hizo, ilikuwa ni baada ya mwezi ndipo Belesa akapata barua kutoka kwa mama yake kuwa wameshindana na mkwewe, na kumwambia ikiwa atataka kumuoa aendelee japo mama yake alisema asihusishwe. Kwa vile binti mwenyewe hakuonekana tena ukawa ndio mwisho wa mahusiano hayo, Belesa akabaki kutunga wimbo huu mzuri.

Bendi ya kwanza ambayo Belesa alijiunga alipoingia katika jiji la Dar es Salaam akitokea Tanga ilikuwa ni Biashara Jazz Band. Bendi hii ilikuwa chini ya uongozi wa Juma Ubao na ilikuwa mali ya Bodi ya Biashara ya Ndani (BIT). Na katika bendi hii Kakere alitunga wimbo wake wa kwanza ulioitwa Clara.

Belesa alihama Biashara Jazz na kujiunga na Dar es Salaam International Orchestra, kundi lililokuwa limekusanya mabingwa wa dansi wakati huo, wakiwemo Marijani Rajabu, King Michael Enoch, Cosmas Chidumule, Joseph Mulenga, Abel Balthazar na wengine wengi.

Akiwa katika kundi hili, sauti ya Belesa inasikika vizuri katika wimbo Magreth. Wimbo uliotungwa na mpiga gitaa la rhythm wa bendi hiyo Ben Petit. Sehemu aliyoimba Kakere awali ilikuwa inaimbwa na Marijani Rajab lakini kiongozi wa bendi Abel Balthazar alishauri kipande kile aimbe Belesa na ndio kumbukumbu tuliyonayo. Wakati yupo Dar es Salaam International alishiriki katika kurekodi nyimbo za bendi yake ya zamani ya Biashara Jazz Band. Alirekodi nyimbo kama Furaha ya Nyani, Shemeji Shemeji, na Afrika Kaburu yee. Jambo ambalo lingekuwa gumu kwa siku hizi, kuwa katika bendi moja na kurekodi nyimbo na bendi yako ya zamani.

Siku moja wakati Dar International ikifanya onyesho Mnazi Mmoja, zamani bendi nyingi zilikuwa zikifanya maonyesho ya mchana bure pale Uwanja wa Mnazi Mmoja, viongozi wa Vijana Jazz, Hassan Dalali na Hamisi Fadhili walimfuata na kumshawishi yeye na Kassim Mponda wajiunge na Vijana Jazz Band, wakapewa ahadi ya uhakika ya ajira na mshahara mnono.

Walihamia Vijana Jazz na kuwepo katika bendi hiyo kwa miezi mitatu, lakini ahadi ya ajira haikutimia wakahamia Juwata Jazz Band.

Belesa akiwa Juwata, pamoja na wimbo wa Sogea Karibu alitunga nyimbo nyingine kama Fukara Hapendezi, Utu ni Tabia Njema, nyimbo hizo awali alikuwa akiimba yeye Belesa lakini siku ya kwenda kurekodi aliumwa ghafla na sehemu alizokuwa akiziimba zikawekwa sauti na marehemu Shaaban Dede.

Wakati huo bendi ya Bima Jazz iliyokuwa mali ya Shirika la Bima la Taifa ilikuwa imedorora, mmoja ya wanamuziki wa Bima, Salum Urembo alitoa wazo kuwa Belesa angeweza kusaidia hivyo akaitwa.

Na bendi ikachangamka kutokana na tungo za Belesa kama vile Remmy, Ombi na Asia. Kwa maelezo ya Belesa mwenyewe Asia na Ombi zilitungwa na mdogo wake Juma Kakere, ambaye wakati huo alikuwa shule, hivyo wakati wa likizo alimpa kaka yake tungo hizo nae akaziwasilisha Bima na zikaja kutingisha ulimwengu wa muziki wakati ule na kuendelea kupendwa mpaka leo.

Ni wakati akiwa Bima ndipo alipoanza kupumzika kufanya shughuli za muziki wa bendi, na kuwa mfanyakazi wa ofisini katika ofisi za Bima. Lakini hamu ya muziki ikamshawishi kuanzisha kundi ambalo liliitwa DJAKABEMPIJU jina lililotokana na herufi za wanamuziki waliokuwemo katika kundi hilo. Dancun, Jafari, Kamala, Belesa, Mponda na Juma. Lakini kabla kundi halijatoa albamu yake ya kwanza wachache waliondoka na kundi kubaki linaitwa DJKABE. Kundi hili lilitoa albamu iliyokuwa na kibao Mama Mona, Belesa alirekodi tena wimbo Sogea Karibu lakini haukupata umaarufu kama ule Juwata.

Belesa Kakere Kakere amefariki usingizini mkesha wa kuamkia Mei, 7 mwaka huu. Mungu Amlaze Pema Peponi.

Chanzo: mwananchi.co.tz