Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIMULIZI ZA MUZIKI: Hakuna wakati msanii Bongo hajaacha kuonekana wa ovyo

50793 Pic+msanii

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki hii mitandao ilitawaliwa na matokeo ya kipande cha hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam. Kati ya maneno aliyoyasema ni kuwa, watu wa ovyo wanakuwa maarufu na watu wa maana hawajulikani hata walipo.

Maneno hayo yameleta gumzo kubwa, wengine wakimtetea mkuu wa mkoa kuwa alichosema ni sahihi na wengine wakimtetea ‘Konki Liquid’ kuwa hajamkosea mtu na Mungu kamjalia alichonacho.

Nimeona walionukuu Katiba ya nchi kumtetea Konki Liquid, wengine wakinukuu Katiba ya Chama cha Mapinduzi kumtetea Konki Liquid, basi mambo yalikuwa motomoto.

Lakini Wahenga walisema, kuishi kwingi kuona mengi. Kutokana na kuishi kwingi, si mara ya kwanza kusikia kundi au watu fulani wakiitwa wa hovyohovyo na wengine kuonekana wa maana katika historia ya nchi hii.

Kwa kundi la wananchi wanaoitwa wasanii, suala la kuitwa au kuonyeshwa kwa vitendo kuwa ni watu wa ovyo ovyo nalifahamu toka nilipoanza kupata akili ya kujitambua kuwa mimi ni msanii huko nyuma miaka ya sabini.

Kwanza nianze kwa kuwashukuru wazazi wangu, walimu wangu wa shule zote za msingi nilizopitia, na baadaye sekondari, hasa mwalimu mkuu wa shule ya Aga Khan pale Iringa marehemu F D Ntemo kwa kutambua kuwa duniani kuna wasanii na si watu wa ovyo ovyo.

Alitupa kila msaada wasanii na hatimaye kutoa nafasi ya wasanii kuonyesha vipaji vyao, kwa wanafunzi wenzetu wa shule yetu na shule za jirani na tukapewa sifa tulizostahili kama walivyopewa walioshinda mashindano ya hesabu au mechi za mpira, na ndivyo ilivyokuwa nilipojiunga na chuo cha ualimu cha Kleruu enzi hizo kikiwa chini ya marehemu F. Basimaki.

Wasanii tulipewa nafasi na kuheshimiwa kama watu wenye vipaji vingine, tulikuwa na bendi ya chuo, nakumbuka kuna watu waliajiriwa kwa kuwa walikuwa wakijua kupiga magitaa na kusaidia kutufundisha utaalamu huo.

Hatimaye nilimaliza masomo na kwa kutumia msamiati wa siku hizi, niliingia mtaani na ngoma ndio ilianza pale. Nianze na kitu ninachokikumbuka ambacho nina uhakika wanamuziki wengi wa zamani walikipitia, nacho ni kulazimishwa kutumbuiza katika shughuli mbalimbali zikiwemo kupokea viongozi, kusindikiza Mwenge na kadhalika. Viongozi wa Serikali walipanga kila kitu wasanii mkatakiwa kutekeleza.

Kabla ya tukio, mngebembelezwa na kuahidiwa usafiri na chakula, fedha hazikutajwa kwa shughuli za kiserikali, tulitakiwa kuwa wazalendo. Hivyo basi wanamuziki na vyombo vyetu tuliletewa usafiri ambao siku hizo ilikuwa lori na humo tulibebwa na kupelekwa tulipopangiwa kupiga muziki.

Baada ya kuanza shughuli huo ndio mara nyingi ulikuwa mwisho wa mawasiliano kati ya watu wa maana na wasanii. Kama kingetolewa chakula ilikuwa bahati, lakini mara nyingine hata usafiri wa kuwarudisha mlikotolewa ulikosekana.

Wasanii tulikuwa wa maana tu pale tulipotakiwa baada ya shughuli tuligeuka kuwa wa ovyo ovyo. Hata siku hizi lalamiko hili bado liko palepale, wakati wa kampeni mbalimbali wasanii ni muhimu, kampeni zikiisha mnageuka tena watu wa hovyohovyo, kama ni wanamuziki mnageuka wapiga kelele mnaesumbua watu, na hakika wanamuziki wengi wameshapambana na polisi wengine hata kutimuliwa kwa mabomu ya machozi usiku kwa kusumbua watu. Nakumbuka siku moja onyesho letu lilikatizwa kwa kuwa tulikuwa tukipiga karibu na nyumba ya kiongozi, ili tusimsumbue.

Ni kiongozi yuleyule tuliyezunguka naye tukimpigia muziki uleule wakati wa kampeni, tulishageuka watu wa hovyohovyo.

Wasanii wachoraji na wachongaji hata kuonekana hawaonekani, hawana mvuto kwenye shughuli za kukusanya watu na ndio maana si ajabu mtu kuona heri atoe tenda ya uchoraji wa nembo ya ndege kwa nchi nyingine, tena kwa bei kubwa sana kuliko kuwapa watu wa hovyohovyo wa hapa nchini tenda hiyo.

Sio siri kuwa somo la sanaa lilitoswa siku nyingi kutoka kwenye elimu ya shule zetu, japokuwa tafiti zinaonyesha kuwa sanaa ni muhimu sana kwa kukuza uelewa wa watoto, lakini hakika kwa wahusika, sanaa ni mambo ya hovyohovyo yasiyostahili kugharamiwa na serikali.

Kutokuwa na somo hilo kuna athari kubwa katika kujenga uzalendo na maadili ndani ya watoto wetu, angalia sanaa zinazothaminiwa na vijana siku hizi, ni sanaa kutoka nchi zilizogharamia watoto wao, nchi yetu inaelekea kuwa wateja tu wa kazi za wasanii wa nje na pia kuwa wateja wa maadili ya zinakotoka sanaa hizo.

Mwaka 1995 baada ya uchaguzi lilitajwa Baraza la Mawaziri, Utamaduni haikutajwa, mwanzoni tulidhani labda imesahaulika kwa bahati mbaya, baada ya muda tukasikia maafisa Utamaduni wa Mkoa wamefutwa, wakafutwa na maafisa wa wilaya, hatimae na Kamishna wa Utamaduni kule juu Wizarani akaondolewa.

Haiihitaji akili ya ziada kujua utamaduni umewekwa katika kundi gani. Katika hotuba ya bajeti mwaka huu, Waziri wa Tamisemi hakutaja utamaduni, japo maafisa utamaduni na sanaa wanasemekana wako chini yake. Na hakika Waziri wa Utamaduni hakutaja Maafisa Utamaduni na sanaa kwani hawako chini yake.

Kubwa kabisa kuonyesha serikali yenyewe inakubaliana kuwa wasanii ni watu wa ovyo ovyo ni kuwa haitaki hata kuweka taratibu sahihi za kukusanya kodi ya kazi zinazotokana na sanaa, wala haina muda wa kusikiliza ushauri namna ya kukusanya kodi hizo. Hebu angalia CD na DVD zisizo na stika za kodi zilivyosambaa nchi nzima!



Chanzo: mwananchi.co.tz