Waswahili wanasema kila jambo lina wakati wake, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa Abdu Hamid, maarufu Kontawa, msanii wa miondoko ya hip hop, ambaye alikuwa na wazo la kuwa mhandisi, lakini akaibukia kwenye muziki.
Ukweli usiopingika Kontawa kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri na ngoma ‘Champion’ aliomshirikisha mkali wa miondoko hiyo Emmanuel Elibariki, maarufu ‘Nay wa Mitego’ huku marudio yake akimshirikisha Rajab Abdul, maarufu ‘Harmonize’.
Kontawa akiwa katika mahojiano na Mwananchi, anaeleza alikopata wazo la kuandika ngoma Champion.
“Nilikwenda Iringa kutumbuiza, nilipopanda jukwaani nilipokelewa kwa furaha na mashabiki wakiimba pamoja nami, ndipo nilivyoamini kuwa mimi ni mshindi ‘champion’, na sio msanii mdogo kama nilivyokuwa najichukulia,” anasema.
Anasema awali hakuwa na wazo la kumshirikisha msanii mwingine, lakini Ney wa Mitego alipousikia akasema angependa aweke mistari kuwa na uhalisia wa maisha yake aliyopitia huko nyuma.
“Kwangu mimi niliona ni kitu kikubwa kutokana na ushawishi alionao Ney, niliamini kupitia yeye wimbo utazidi kwenda mbali.
“Lakini mwisho wa siku kitu kilichotoka kilikuwa ni kikubwa, kwani hata mimi nilionekana sijabebwa kutokana na aina ya mistari niliyoiandika ilikubalika,” anasema Kontawa.
Anasema aliamua kufanya marudio ya wimbo huo na Harmonize kwa sababu ya ukubwa aliokuwa nao katika muziki.
“Alinitumia meseji katika mtandao wa Instagram kunieleza anataka tufanye kitu katika huu wimbo, nataka ufike mbali kwa sababu una kipaji na unafanya vizuri, maneno hayo yalitosha mimi kukubaliana naye na tukaurudia,” anasema.
Ilikuwaje akaingia kwenye muziki
Kontawa anasema kuwa aliingia kwenye muziki baada ya kukaa nyumbani muda mrefu bila shughuli yoyote.
“Malengo yangu ilikuwa kuendelea na chuo baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2014, akilini kwangu nilikuwa ninatamani kuwa mhandisi wa majengo, kwa bahati mbaya sikupata fedha ya kwenda kusomea mambo hayo.
“Nikaanza kuuza nguo za mitumba na kufanya kazi viwandani, lakini sikuwa napata fedha ya kutosha, ndiyo maana nikaamua kujikita kwenye muziki,” anasema.
Anasema baada ya kutoa vibao kama ‘Sura ya baba’, ‘Mwanamke’, ‘Moyo’, ‘Mke’ na ‘Shetani akisafiri’, alipokelewa vizuri kwenye uga wa hiphop.
Nje ya hiphop anatamani kufanya nini?
Kontawa anasema ana wazo kufungua kampuni itakayojihusisha na mambo ya mapambo ya nyumba, kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuwa mhandisi katika ujenzi na bado inaishi ndani yake.
Anawafikishiaje mashabiki alichokiandaa?
“Nauza muziki wangu kwenye mitandao kama boomplay, sportfy kwa sababu fedha unayoipata kule ni tofauti na yule anayeuza moja kwa moja.”
Familia
Kontawa ni mtoto wa tatu kati ya watano wa mzee Hamid.
“Kuhusu maisha yangu binafsi napenda zaidi ibaki kuwa siri yangu, nataka mashabiki wanijue zaidi kupitia kazi na si vinginevyo.
“Mashabiki wangu wakae mkao wa kula, najipanga kuachia ngoma nyingine na ninawaahidi mwaka ujao nitaachia ngoma baada ya ngoma, hakuna kulala, ni mwenzo wa burudani,” anasema Kontawa.