Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msanii asema, nilidhani nimerogwa kumbe TB

61734 Pic+msanii

Sun, 9 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Nilidhani nimerogwa baada ya kuugua bila kupata ahueni kwa kipindi fulani, ilibidi niende kwa mganga wa kienyeji kupata tiba.

“Hata hivyo, sikupona na niliendelea kudhoofika, baadaye dada yangu (marehemu) akanishauri niende hospitali, ndiyo wakabaini naumwa Kifua Kikuu (TB).”

Hivi ndivyo msanii wa ngoma za asili kutoka kikundi cha Mukikute jijini Dar es Salaam, Gota Ngogota alivyokuwa akizungumzia TB baada ya kupata matibabu halisi kutoka hospitali na kupona.

Simulizi ya Ngogota

Awali, Ngogota aliamini kuwa amerogwa kwa sababu homa zilizokuwa zinamkumba hakujua zinasababishwa na nini.

Aliamua kwenda kwa waganga wa jadi kupata tiba akijua afya yake itatengemaa na kuendelea na maisha kama kawaida kwa sababu dalili alizokuwa anapata alijua zinatokana na ‘nguvu za giza.’

Pia Soma

“Zilianza dalili za kawaida tu, nikajua ugonjwa wa kawaida lakini baadaye nilishangaa napata joto kali, nakohoa mfululizo na usiku natoka jasho jingi sana nikajua nitakuwa nimerogwa siyo bure,” anasimulia Ngogota.

Anasema alipokwenda kwa mganga alipewa dawa na aliambiwa angepona baada ya kutumia dawa hizo lakini hali iliendelea kuwa mbaya.

“Basi dada yangu ambaye kwa sasa amefariki, aliponitazama akasema hapana itabidi niende hospitali; hivyo nikakubali kwenda kutibiwa hospitalini na nilipopimwa waligundua ninaumwa TB,” anaeleza kijana huyo ambaye kwa sasa ameamua kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha vijana wengine kuhusu ugonjwa huo.

Anasema alianza matibabu na baadaye afya yake ilianza kutengemaa, “kwa hiyo nilikunywa dawa kama nilivyoelekezwa na nilipomaliza miezi sita nilipona kabisa. Nachofanya sasa ni kuwaelimisha wenzangu wakiona dalili kama nilizoona mimi wakimbie hospitali, wasifikirie kuwa wamerogwa.”

Awali, Ngogota alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa ushiriki wa wadau katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo unaojulikana kwa jina la ‘Stop TB Partnership.’

Mkutano huo ulioandaliwa na Health Promotion Tanzania wakishirikiana na Serikali unalenga kuwashirikisha wadau wote katika mapambano dhidi ya TB.

Baadhi ya wadau muhimu kwenye mapambano hayo ni mashirika, taasisi na asasi za kiraia, waganga wa jadi na viongozi wa dini na jamii kwa ujumla lengo likiwa ni kuibua, kuwapima na kuwapatia matibabu wagonjwa wa kifua kikuu.

Hali halisi kuhusu TB

Ukweli ni kwamba wapo baadhi ya watu hukimbilia kwa waganga wa kienyeji kupata tiba wanapojisikia kuumwa badala ya kwenda hospitali kupima na kujua kama wanaumwa TB au ugonjwa mwingine.

Utafiti uliofanywa mwaka jana na Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, ulionyesha kuwa waganga wa jadi wapo hatarini kupata ugonjwa huo kwa sababu hupokea wagonjwa wengi.

Hiyo inamaanisha baadhi ya wagonjwa hawapati tiba sahihi ya ugonjwa huo jambo ambalo ni hatari kwa sababu wanaweza kuambukiza wengine.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu anasema takwimu zinaonyesha kuwa watu watatu wanafariki dunia kila baada ya saa moja nchini kwa sababu ya TB sawa na idadi ya watu 70 kila siku.

Pia, takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha asilimia 56 ya wagonjwa wa TB hawajagunduliwa wakati, wataalamu wa afya wakisema mtu mmoja ambaye hajagundulika anaweza kuambukiza watu 10 mpaka 20 kwa mwaka.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari anasema Tanzania ni kati ya nchi 30 zinazotajwa kuwa na maambukizi makubwa ya TB.

Ummy anasema kihalisia ugonjwa huo ndiyo unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani na kwamba mtu yeyote anaweza kuambukizwa.

Anasema TB ni vita inayotakiwa kupigwa na kila mmoja kuanzia ngazi ya kaya mpaka Taifa.

“Ushirika huu unahitaji pia waganga wa jadi kwa sababu wao wanapokea wagonjwa wengi sana na wapo hatarini kuambukizwa,” anasisitiza Waziri huyo wa afya.

Anasema mbali na waganga, viongozi wa dini ni watu muhimu katika vita dhidi ya TB kwa sababu wanaweza kutumia walau dakika moja kwenye kila mahubiri yao kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huo.

“Wanaweza kuwa wanawaambia TB inatibika hivyo badala ya kuhangaika wanapoona dalili hizo waje hospitali watibiwe, TB inatibika,” anasisiriza Ummy.

Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Beatrice Mutayoba anasema TB inawapata zaidi wanaoishi katika mazingira magumu, msongamano wa watu na wanaokaa karibu na wagonjwa.

Anayataja makundi yaliyo hatarini kuwa ni watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU), watoto na wazee.

Anaeleza kuwa wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, inaendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya Serikali na vituo binafsi.

Dk Mutayoba anasema utekelezaji wa mpango huo umeleta mafanikio mbalimbali na kuvuka malengo ya mwaka 2018 kwa kuwafikia wagonjwa 75,845 ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015.

Mikakati ya kutokomeza TB

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari anasema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kupambana na ugonjwa huo lakini kila mdau lazima ashiriki kwenye jambo hilo kutokomeza.

Hata hivyo, Waziri Ummy anasema pamoja na ukubwa wa tatizo hilo kila mdau akishiriki mapambano dhidi ya TB, ataweza kusaidia kuwafikia wagonjwa wengi zaidi ambao hawajaibuliwa.

Waziri Ummy anasema ‘Stop TB Partnership’ ilianza kutekelezwa kwenye nchi nchi nyingine tangu mwaka 2001 kama mkakati wa kimataifa wa kushirikisha wadau katika kupambana na ugonjwa huo.

Anasema tayari nchi saba ikiwamo Tanzania zimeshaunda ushirika huo unaoweza kuwa suluhisho la kufikia asilimia 90 ya wagonjwa kuibuliwa na kupata tiba.

Mipango mingine iliyotekelezwa na Serikali katika kupambana na kifua kikuu ni Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015-2020) wenye lengo la kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 2o.

“Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo kwa vituo vya Serikali na binafsi,” alisema Ummy.

Anasema wameweza kuvuka lengo kwa kuwafikia wagonjwa 75,845 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015.

Dalili za kifua kikuu

Dk Mutayoba anasema ni rahisi mtu anayeishi na VVU kuambukizwa kifua kikuu. Anasema ugonjwa huo unaoshambulia mapafu ndiyo unaoongoza kwa kuua watu walioambukizwa VVU ikiwa hawataanza matibabu mapema.

Dalili za kifua kikuu kukohoa zaidi ya wiki mbili, kikohozi sugu na kukohoa damu, homa kutokwa jasho usiku na kukonda.

Waziri Ummy anasema dalili hizo huhitimishwa na kipimo cha hospitali hivyo ni vizuri mtu akihisi hivyo awahi kupata tiba.

Chanzo: mwananchi.co.tz