MCHEZAJI wa kimataifa wa Yanga, Benard Morrison ameiingizia Yanga Sh.30 milioni, baada ya jezi zake kuuzwa kama njugu kwenye mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga uliopigwa Machi 8 Jijini Dar es Salaam.
Nyota huyo anayetamba kwa sasa na kukubalika ndani ya Wanajangwani hao, anakuwa mchezaji mwenye mauzo makubwa zaidi ya Yanga kwenye miaka ya karibuni. Lakini vilevile tafsiri nyepesi ni kwamba mauzo hayo yana uwezo wa kulipa posho za mechi tatu zijazo za ushindi Yanga ambazo kila wakishinda wanapewa Sh. 10 milioni.
Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema mchezaji huyo aliongoza kwa mauzo ya jezi baada ya jezi zake 1,500 kuuzwa katika mchezo huo aliofunga bao pekee dakika ya 44.
Nugaz alisema katika mauzo hayo ya Sh 20,000 ambayo ilikuwa bei elekezi inayoendelea wiki nzima Yanga ilipata mapato hayo na bado inaendelea kuuza jezi ya nyota huyo.
“Awali tuliandaa jezi 1,000, wakaja watu wanaoomba tuwatengenezee jezi ya huyu mtu, tukaziandaa nyingine 500 na zote ziliisha. Jezi ya pili kwa mauzo ilikuwa ni ya Tshishimbi, kwani naye kabla ya mchezo huo tuliuza zaidi ya jezi zake 400,” alisema Nugaz ambaye maneno yake ya shombo yamekuwa yakiwakera Simba mitandaoni.
Aliongeza kuwa wachezaji wengine ambao jezi zao zinauliziwa zaidi ni Ditram Nchimbi na Mapinduzi Balama.