Tume ya Utangazaji Zanzibar imepiga marufuku kwa Vituo vyote vya Utangazaji (Radio na TV) ikiwemo mitandao ya kijamii, kuchezwa, kupigwa na kutumika katika Vituo vyote vya Utangazaji, ikiwemo pia kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wimbo wa ‘Malaya Twajuana' ulioimbwa na Wasanii tofauti wa nje ya Zanzibar akiwemo Msanii wa Taarab wa Zanzibar, Jaffar Bai.
Tume hiyo imesema miongoni mwa majukumu yake ni kudhibiti na kusimamia shughuli za Utangazaji Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kulinda sera, usalama, mila ma utamaduni wa Zanzibar usiharibiwe.
Tume ya Utangazaji Zanzibar, kwa Mamlaka ya kisheria iliyopewa chini ya kifungu cha 16(e) cha Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar Nambari 7 ya 1997, imesema haitasita kuchukuwa hatua za kisheria kwa kituo chochote cha Utangazaji, au mtu yoyote atakaekiuka agizo hili.
“Tume ya Utangazaji Zanzibar, inaendelea kuviasa vituo vya Utangazaji vinavyofanya kazi Zanzibar, kufuata masharti ya leseni waliyopewa pamoja na maadili ya habari sambamba na kutunza mila silka na utamaduni wa Wazanzibari”