Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kupanda Na Kushuka Kwa Defao Mpaka Kifo

Defao Afrikaaaa Kupanda Na Kushuka Kwa Defao Mpaka Kifo

Thu, 30 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamuziki mahiri na mkongwe wa Rhumba kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, General Defao amefariki dunia Desemba 27, 2021 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Laquintinie huko Douala, Cameroon, ambako alikuwa amelazwa.

Defao ambaye jina lake halisi ni Lulendo Matumona, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi, akiwa na umri wa miaka 62 huku ugonjwa wa kisukari ukitajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kifo chake.

Ifuatayo ni historia fupi ya Defao, kuanzia kuzaliwa, jinsi alivyoingia kwenye muziki na kupata umaarufu mkubwa na baadaye kushuka mpaka alivyofikwa na mauti.

Defao alizaliwa Desemba 3, 1958 katika Jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aliianza safari yake ya kimuziki mwaka 1976 baada ya kujiunga na bendi ya mtaani kwao katika mitaa ya Jiji la Kinshasa ambapo alianza kuimba, huku akivutiwa zaidi na wasanii Papa Wemba, N’Yoka Longo, Gina Efonge na Evoloko ambao kwa wakati huo walikuwa wakiunda Kundi la Zaiko pamoja na mkongwe Tabu Ley Rochereau.

Mwaka 1978, alijiunga na Bendi ya Orchester Suka Movema, baadaye akahamia Fogo Stars na Somo Westambako hakudumu sana.

Ndoto zake zilianza kutimia mwaka 1981 ambapo kipaji chake kilionwa na mpiga gitaa wa Kundi la Le Grand Zaiko Wawa, Felix Manuaku ambaye aliwashawishi wenzake wamchukue kwenye bendi yao.

Akiwa ndani ya Bendi ya Le Grand Zaiko Wawa, ndipo nyota yake ilipoanza kung’ara zaidi ambapo sauti yake nzuri pamoja na namna alivyokuwa akicheza, vilimpaisha na kumfanya aanze kuwa gumzo.

Baada ya kupata mafanikio makubwa akiwa katika kundi hilo, mwaka 1983 alijitoa kwenye kundi hilo na kwa kushirikiana na mwanamuziki mwenzake wa Rhumba, Bozi Boziana, walianza kundi jipya la Choc Stars.

Aliendelea kufanya vyema na Kundi la Choc Stars ambapo mwaka 1991, aliamua kuachana na kundi hilo na kuanzisha kundi lake la The Big Stars akiwa na Djo Poster.

Nyota yake iliendelea kung’ara zaidi akiwa na kundi lake la Big Stars ambapo katika kipindi cha miaka mitano tu, alitoa albamu takribani 17 na sita kati yao, zilifanikiwa kupenya hadi katika soko la muziki barani Ulaya.

Ni katika kipindi hicho, ndipo Defao alipoanza kupambanishwa na magwiji wengine katika muziki wa Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akiwemo Papa Wemba, Koffi Olomide na wengine wengi, jina lake likazidi kuwa kubwa duniani kote.

Kama ilivyoelezwa, kingine kilichomfanya azidi kuwa kivutio cha wengi, ni jinsi alivyokuwa akilisakata rhumba na Sebene kwenye video za nyimbo zake kwa wepesi licha ya kuwa na umbo kubwa, akazidi kupendwa.

Katikati ya miaka ya 1990, Defao alikuwa tayari akitishia kufuta majina maarufu katika muziki wa Dansi wa DR Congo kama Koffi Olomide na Bozi Boziana kutoka ulingo wa muziki lakini hakufaulu kupata umaarufu nje ya nchi.

General Defao ni mwanamuziki aliyekuwa na kipaji cha kutunga na kuimba nyimbo kwa sauti nyororo na yakuvutia kwa wapenzi wa Rhumba. Alijizolea umaarufu mkubwa kwa miondoko yake ya Ndombolo na Ikibinda Nkoi aliyoiimba.

Aliweza kutambulika rasmi kwenye tasnia ya muziki wa Rhumba mnamo mwaka wa 1976, wakati alipotoa nyimbo kubwa kama School of Love, Kikuta Family, Nadine, Bolingo na Sidewalk.

Watanzania wanamkumbuka Defao alipotembelea na kufanya shoo nchini ambapo alikuwa akitumbuiza kwenye ukumbi wa Imasco Center ulio karibu na Uwanja wa Uhuru na Dj wa ukumbi huo enzi hizo Dj Makay na mkongwe Dj Jerry Kotto akawa anaendeleza ngoma zake kila wiki ukumbinu humo baada ya Defao kuondoka nchini.

Hata hivyo, kukosekana kwa menejimenti imara ya kusimamia muziki wake, kunatajwa kuwa sababu kubwa iliyofanya umaarufu wake kuanza kupungua kwa kasi kubwa mwishoni mwa miaka ya 1990.

Matatizo mbalimbali yalianza kujidhihirisha kwenye kazi zake, kama maandalizi hafifu ambayo yalisababisha awe anabadilisha mapryodyuza wa nyimbo zake mara kwa mara, wakati mwingine akiachia nyimbo ambazo hazikuwa na usikivu mzuri au kuachia wimbo mmoja kutoka lebo mbili tofauti za muziki.

Ilipofika mwaka 2000, tayari giza lilishatanda kwenye ‘career’ yake ya muziki, nyimbo zake mpya zikawa hazipati umaarufu kama ilivyokuwa mwanzo na hatimaye, aliamua kulivunja Kundi lake la Big Stars na kuhamishia makazi yake jijini Paris, Ufaransa.

Akiwa jijini Paris, alianda albamu nyingine ya Nessy de London na kwa msaada mkubwa wa wasanii wenzake wa Rhumba kama Nyboma Mwana Dido, Luciana De Mingongo, Wuta Mayi, Ballou Canta na Deesse Mukangi aliowashirikisha kwenye albamu hiyo, nyota yake iliang’ara upya na kuifanya albamu hiyo kupendwa na wengi.

Hata hivyo, Waswahili wanasema la kuvunda halina ubani, licha ya albamu hiyo kufanya vyema, Defao alijikuta akiingia matatizoni na serikali ya DRC ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ikiongozwa na Rais Joseph Kabila!

Haifahamiki ni nini hasa kilichokuwa chanzo cha kuingia matatizoni na serikali lakini baadaye alizuiliwa kurudi nchini humo na nyimbo zake zikawa hazipigwi tena ndani ya mipaka ya DRC, akahamishia makazi yake jijini Nairobi, Kenya!

Huo ukawa mwanzo wa safari nyingine ya kuporomoka kimuziki ambapo aliishi maisha ya kutangatanga uhamishoni kwa muda mrefu na mwisho akafilisika kiasi cha mara kadhaa kujikuta akikamatwa na polisi kwa madeni ya hoteli alizokuwa akiishi akiwa uhamishoni nchini Kenya.

Nchini Kenya aliwahi kufungwa miezi sita kutokana na madeni ya hoteli aliyokuwa akikaa bila kulipa kwa ukosefu wa fedha. Alitokea msamaria mmoja akamlipia deni hilo na Defao akawa huru.

Baada ya takribani miaka 6, mwaka 2006 Defao alijitutumua na kutoa albamu nyingine aliyoipa jina la Nzombo ambayo nayo haikufanya vizuri, mwaka 2010 akatoa nyingine ya Pur ambayo ilikuwa ni kama msumari wa mwisho kwenye jeneza lake.

Wachambuzi wa masuala ya muziki, wanaeleza kwamba albamu hiyo ilishindwa kurekodiwa kwenye CD na kubakia mitandaoni tu kutokana na ubora wake hafifu.

Mwaka 2012 alirudi tena na albamu nyingine ya Undertaker ambayo nayo ilibuma na mwaka 2016, akatoa nyingine ya Any Time, nayo ikaangukia pua.

Mwaka 2019, Defao aliamua kurejea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kuishi kwa takribani miaka 21 uhamishoni na akaanza upya kujitafuta kimuziki, safari hii akiwa chini ya mwalimu wake wa tangu ujanani, Montana Kamenga lakini kwa bahati mbaya zaidi, Janga la Corona liliikumba dunia na kufanya shughuli zote za kimuziki kusitishwa nchini humo na sehemu nyingine nyingi duniani kote.

Mpaka anafikwa na umauti, Defao alikuwa ameshindwa kabisa kurejea kwenye ubora wake!

Taarifa za kifo chake, zimepokelewa kwa hisia tofauti, ambapo wasanii wakubwa nchini humo kama Ferre Gora na Fally Ipupa ni miongoni mwa waliotoa salamu za rambirambi na kusikitishwa na jinsi kipaji kikubwa alichokuwa nacho Defao, kilivyopotea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live