Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kolabo Kali Zilizotikisa Zaidi Bongo 2021

DIAMONDZZ Kolabo Kali Zilizotikisa Zaidi Bongo 2021

Thu, 30 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WASANII kufanya kazi kwa ushirikiano (kolabo) na wasanii wengine ama kutoka ndani au nje ya Tanzania ili kutengeneza kazi nzuri, ni jambo bora zaidi kwa maendeleo ya muziki wa Bongo Fleva.

Kwa mwaka 2021, zilisikika ngoma kali na nyingi mno za pamoja, lakini zipo ambazo zimeachiwa na wasanii kutoka nchini Tanzania kwa mwaka huu na kutikisa vilivyo;

BAIKOKO - MBOSSO FT DIAMOND PLATNUMZ

Hii ni moja kati ya kolabo kali zilizotesa zaidi kwa mwaka 2021 na hii ni kutokana na ushirikiano mzuri ulioonekana baina ya Mbosso na bosi wake kunako Lebo ya Wasafi, Diamond Platnumz.

NDOMBOLO - ALI KIBA FT ABDU KIBA & TOMMY FLAVOUR

Hii ni ngoma ambayo inaonesha wazi ufundi na uwezo mkubwa walionao memba wa Lebo ya Kings Music chini ya King Kiba kwenye suala zima la utunzi na uandishi wa muziki. Kolabo hiyo iliwaweka pamoja wasanii wote walio chini ya Kings Music.

EX WANGU REMIX - SENETA KILAKA FT HAMISA MOBETO

Ex Wangu Remix ni moja kati ya ngoma za Singeli ambazo zimepamba mno mwaka 2021. Hii imechagizwa na wazo zima la wimbo kuwa la kibunifu pamoja na ushirikiano mzuri wa kisanaa uliooneshwa kati ya damu mpya kwenye gemu, Seneta Kilaka na mwanamama Hamisa Mobeto.

BEER TAMU - MARIOO FT TYLER ICU, VISCA & ABBAH PROCESS

Huwenda ikawa ndiyo ngoma ya Amapiano iliyotamba zaidi Bongo kwa mwaka 2021. Hii ni kutokana na namna ambavyo Marioo ameimba vizuri kwenye ngoma hii akitumia mdundo wenye nguvu ambao umetayarishwa na Abbah Process na Tyler Icu.

KUSHKI - CHEGE FT SARAPHINA

Ushirikiano mzuri kati ya Chege na Saraphina kwenye Kushki umesababisha ngoma hii kuwa na uraibu wa kupitiliza hasa kwenye sehemu ya kiitikio ambacho Chege ameweza kukitendea haki.

LALA - RAYVANNY FT JUX

Ngoma hiyo iliweza kumkutanisha Rayvanny ambaye husifika kwa uwezo mkubwa wa kuimba pamoja na Jux ambaye wengi humsifu kwa sauti yake ambayo hutaradadi mno kwenye muziki wa RnB.

UNAUA VIBE - RAPCHA FT YOUNG LUNYA & DWIN

Moja kati ya kolabo bora zaidi ya Hip Hop Bongo kwa mwaka 2021. Hii ni kutokana na shauku ya mashabiki kuwa na hamu ya kumsikia Rapcha na Young Lunya kwenye ngoma moja. Baada ya ngoma hii kufanya vizuri Bongo, miezi minne baadaye Rapcha aliachia Unaua Vibe Remix akiwashirikisha Femi One na King Kaka kutoka Kenya.

FOR YOUR LOVE - MBOSSO FT ZUCHU

Hii ni ngoma ambayo imezidi kuthibitisha uwezo wa Mbosso kwenye uandishi wa ngoma na uwezo alionao Zuchu kwenye kuimba pale anaposhirikiana na Mbosso.

Kupitia mitandao ya kijamii kama Tikitok, Instagram na Snapchat mashabiki wengi hasa wa kike wameonekana kuvutiwa mno na ngoma hii.

IYO - DIAMOND PLATNUMZ FT FOCALISTIC, MAPARA A JAZZ & NTOSH GAZI

Kupitia kolabo hiyo, Diamond Platnumz amezidi kudhihirisha anaweza kufanya kazi na msanii anayeimba aina yoyote ya muziki barani Afrika.

JEALOUS - ALI KIBA FT MAYORKUN

Kutoka kwenye albam yake ya Only One King, Ngoma ya Jealous haikufanya vizuri tu Bongo, bali kila upande wa Afrika hasa ukitegemea kuwa ilikuwa ni moja kati ya ngoma chache ambazo King Kiba alishirikiana na msanii kutoka nje ya Afrika Mashariki; yaani Nigeria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live