Wakati wasanii wengine wakipambana kujiweeka rekodi za kipekee kwenye kiwanda cha muziki Duniani wapo wengine kwao ni muda wa kubwaga manyanga na kufanya mambo mengine.
Jambo ambalo linaweza lisiingie kichwani kirahisi kutokana na ahadi nyingi za wasanii wenye kusema wanaacha muziki kushindwa kutimia na baadaye kuwaona tena nyuma ya kipaza.
Nje ya matarajio ya mashabiki wake, Msanii mahiri wa muziki wa Hip Hop kutokea nchini Marekani Jordan Michael Houston III maarufu Juicy J ameamua kuweka wazi kuwa kwa sasa yuko tayari kuachana na muziki na kujikita na shughuli nyingine.
Juicy J mwenye umri wa miaka 46, ametangaza rasmi taarifa hizo za kuacha muziki kupitia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa twitter ambapo amesema kuwa kwa sasa ataziingiza sokoni album zake mbili kwanza baada ya hapo hatajihusisha tena na muziki.
Juicy J anayo historia ya kufanya kazi na mstaa kadhaa akiwamo Wiz Khalifa chini ya Tylor gang Music Label, Lil wayne, Usher Rymind, 2 Chainz na wengine wengi.
Kwa kipindi chote alichokuwepo kwenye tasnia ya muziki amefanikiwa kuziingiza sokoni album 5 na jumla ya nyimbo 49.