Msanii wa Bongofleva kutoka Konde Music Worldwide, Harmonize katika harakati za kuhakikisha lebo yake hiyo inakua na kuleta ushindani wenye tija katika tasnia, anajikuta akinasa kwenye mtego uliowahi kumliza Diamond Platnumz.
Septemba 2020 Harmonize alimsaini Country Boy Konde Music wakati huo lebo hiyo ikiwa tayari na wasanii wengine kama Cheed na Killy waliotoka Kings Music ya Alikiba, pamoja na Young Skales wa Nigeria.
Hata hivyo, Januari 2021 Konde Music wakatangaza kuachana na Country Boy kwa madai mkataba wake umemalizika na wamefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kutoendelea kufanya kazi.
Utakumbuka Country Boy alisaini Konde Music tayari akiwa msanii mkubwa ambaye amekuwepo kwenye muziki muda mrefu kabla ya hata ya Harmonize.
Huo ndio mtego uliomnasa na Diamond pale alipomsaini Rich Mavoko ndani ya WCB Wasafi hapo Juni 2016 akiungana na wasanii wengine wa lebo hiyo kwa wakati huo kama Harmonize, Rayvanny na Queen Darleen.
Julai 2018 Rich Mavoko aliamua kuondoka katika lebo hiyo kwa mvutano mkali na mabosi wake hao hadi kufikishana Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa ajili ya usuluhishi.
Katika historia, Mavoko ni msanii wa kwanza kuondoka katika lebo hiyo kama ilivyo kwa Country Boy na Konde Music.
Rich Mavoko kabla ya kusaini WCB tayari alikuwa ni msanii mkubwa hadi kufikia hatua ya kushindanishwa na Diamond.
Kabla ya kuanzisha Konde Music, Harmonize alikuwa chini ya WCB Wasafi yake Diamond iliyomtoa kimuziki mwaka 2015 akiwa ni msanii wa kwanza kusaini.
Baada ya kuondoka WCB, Oktoba 2019 ndipo Harmonize alipotangaza kuzaliwa kwa Konde Music, huku Ibraah akiwa msanii wa kwanza kumsaini pamoja na kuachia EP yake, Steps yenye nyimbo tano.
Kwa muktadha huo utaona Diamond na Harmonize wameshindwa kudumu na wasanii waliowasaini katika lebo zao ambao tayari walikuwa wametoka kimuziki.
Hata hivyo, Harmonize alikuwa na nafasi ya kuepuka hilo kwa kujifunza kwa bosi wake huyo wa zamani.