Mchekeshaji kutoka nchini Kenya Eric Omondi ameweka masharti magumu ambayo mapromota na waandaaji wa matamasha ya muziki nchini humo ni sharti wafuate wakati wa kuandaa hafla na matamasha mbali mbali kuanzia mwaka huu 2022 nchini Kenya.
Kwa mujibu wa mchekeshaji huyo, wasanii wote watakaoalikwa kwa kutumbuiza matamasha lazima walipwe kiasi kisichopungua 75% ya kiwango cha pesa walichokubaliana kabla, na 25% iliyobaki siku ya tukio.
Omondi aliorodhesha idadi ya wasanii wa daraja ‘A’ ambao kamwe hawapaswi kulipwa chini ya Ksh 600k ambayo ni sawa na zaidi ya Milioni 12 za Kitanzania kwa kila onyesho moja.
“Tafadhali ifahamike kuwa mwaka huu binafsi nitachunguza kwa undani kila tukio!!! nataka kujua wasanii wanalipwa kiasi gani.
Ninataka kuhakikisha kuwa kila msanii analipwa asilimia 70 ya pesa zake kabla na asilimia 25 siku ya tukio, hasa kabla ya kupanda jukwaani kutumbuiza, kila msanii kwenye orodha lazima alipwe si chini ya Ksh 600K Kwa wasanii wa daraja A, ninamaanisha wasanii wafuatao.
Nadia Mukami – KSH 600,000, Khaligraph Jones milioni 1.5, Otile Brown Ksh Miliomi 1.5, Nyashinski Ksh Milioni 1.5, Sauti sol Ksh Milioni 2.8.” Inasomeka sehemu ya post ya Omondi.
Baada ya hapo aliongeza kuwa wasanii wote wa daraja ‘B’ wanapaswa kulipwa Sh450, 000 na zaidi kwa kila show moja, akitoa mfano wa rapa chipukizi na nyota wa muziki wa Gengetone, Trio Mio.
“Wasanii wote wa daraja ‘B’ lazima walipwe si chini ya ksh 450K yaani Ethic, Trio Mio n.k. Matukio yote lazima yawe na headline na msanii wa Kenya iwe Beyoncé anatumbuiza au la!!! Usalama lazima utolewe kwa wasanii wote.” aliongeza.
Kauli hiyo ya Omondi imekuja kufuatia muendelezo wa kampeni aliyoianzisha kwa dhamira ya kuwapigania wasanii wa Kenya akihitaji takribani 75% ya muziki wa wasanii wa Kenya kuchezwa kwenye vituo vya redio na TV ili kutoa nafasi kwa wasanii hao kufanikiwa kwa kiwango stahiki.