Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EP ya Diamond yaibua jambo, Harmonize atajwa

Diamond FOA EP 3 Diamond Platnumz

Thu, 17 Mar 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kwa mwezi huu pekee Bongofleva imepokea albamu moja na Extended Plalist (EP) mbili ukiwa ni mwanzo mzuri wa kuifikia na hata pengine kuivunja rekodi ya mwaka jana ambapo muziki huo ulipokea albamu na EP zaidi 10 kwa kila upande.

Dadahood wameachia albamu yao ya kwanza, ‘The Orange’ ikiwa na nyimbo 10, Diamond Platnumz, EP ‘First of All’ (FOA) ikiwa na nyimbo 10, H. Baba, EP, ‘Duku Duku’ ikiwa na nyimbo 12.

Hata hivyo, kumekuwepo na mjadala unaodai kuwa baadhi ya EP hazina sifa hiyo bali zinapaswa kuwa Long-Playing Record (LP), pia baadhi ya albamu hazina sifa hiyo bali zinapaswa kuwa mixtape.

Kabla ya Diamond hakuna msanii wa Bongofleva aliyewahi kutoa EP yenye nyimbo 10, EP ya Ravanny, ‘Flowers’ ndio ilikuwa inashikilia rekodi ya kuwa na nyimbo nyingi zaidi zikiwa nane, huku EP ya K2ga kutoka King Music, ‘Safari’ ikiwa nyimbo chache zaidi ambazo ni tatu.

EP za ‘First of All’ (FOA) na ‘Duku Duku’ kutoka Diamond na H. Baba ndizo hasa zimeacha maswali kutokana na idadi  ya nyimbo ambazo ni 10 hadi 12.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Fahamu Muziki, Frank Daxx amesema albamu, EP na mixtape zinatofautishwa kwa idadi ya nyimbo, dakika za nyimbo zote kwa ujumla na lengo kuu la kimaudhui.

Amefafanua kwa kawaida albamu inatakiwa iwe nyimbo kuanzia nane na kuendelea, muhimu zaidi inapaswa kuwa na mtiririko wa kimaudhui unaoshabihiana (theme) kutoka wimbo wa kwanza hadi wa mwisho.

Amesema msikilizaji anakuwa kama anasoma kitabu kinachoelezea jambo fulani toka ukurasa wa mwanzo hadi wa mwisho.

"Sasa wasanii wetu wanakusanya ngoma zao kadhaa kali wanatoa wanasema ni albamu, ukisikiliza hakuna muunganiko kati ya wimbo na wimbo, pia unakuta hakuna Intro, maana Intro anakuelezea hii albamu inazungumzia kipi hasa," anasema Frank.

Amesema kutokana na albamu kuwa na kigezo hicho kinachowabana wasanii, ndipo wengi wamekimbilia kutoa EP na mixtape ambazo haziwabani kivyovyote vile.

"EP inatakiwa iwe na nyimbo kuanzia tatu hadi nne, zisizidi sita, LP inakuwa ndefu kuliko EP ya kawaida. Hii ya Diamond nasema ni LP kwa sababu ina ngoma nyingi halafu ina dakika zaidi ya 30, zipo kama 33 hivi" anasema Frank.

Ameeleza mixtape inakuwa na mchanganyika wa nyimbo zisizo na idadi maalumu, haina lengo kuu la kimaudhui, ni sehemu ya msanii kuonyesha ubora wake, haimbani, anaweza kusampo ngoma za wasanii wengine na gharama nafuu kuiandaa.

"Ndio maana huwa nasema ile ‘Afro East’ ya Harmonize sio albamu ni mixtape maana kasampo nyimbo nyingi na haina mtiririko maalumu, kila wimbo upo kivyake tu" amesema.

Amesema mara nyingi EP na mixtape huwa zinatoka kwa muktadha wa utambulisho wa albamu na sio kibiashara, kwa nchi ambazo muziki wao umepiga hatua EP na mixtape zinagawiwa bure kwa mashabiki, ni wachache sana huwa wanauza.

"Ukisoma historia za wasanii kama kina Lil Wayne wana mixtape nyingi lakini wewe huzijui kwa sababu wanatoa kwa ajili ya watu mitaani na hii wanafanya kwa zile nyimbo wanazoona sio nzuri kibiashara ila zinasikilizika" amesema Frank  Daxx.

Ikumbukwe kwa Tanzania wasani wenye albamu nyingi ni Mr. II 'Sugu', Lady Jaydee, Soggy Doggy na Juma Nature, huku Rayvanny akiongoza kwa EP, naye Wakazi akitawala upande wa mixtape.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz