Mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz amesema hapendezwi kushindanishwa na wasanii nchini kutokana na kuwazidi katika maeneo makuu matatu; ambayo ni mauzo, shoo za kimataifa na maendeleo (mali) yatokanayo na muziki.
Je, kauli hiyo inasadifu muziki wa msanii huyo kwa kiasi gani? Makala hii inakwenda kuangazia hilo kwa kina, tena kwa mtindo wa namba ambazo kamwe hazidanganyi!
Diamond, aliyetoka kimuziki mwaka 2009 ameshinda tuzo za kimataifa kama Channel O, MTV, Soundcity, Headies, Afrima, Kora, AEA, EAUSA, the HiPipo Music Awards n.k na kumfanya kuwa msanii pekee Bongo kufikia mafanikio hayo kwa kipindi cha miaka 10.
Anashikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2014 kwa usiku mmoja, anakaribiwa na Alikiba aliyeshinda tuzo tano mwaka 2015, ikiwa ni sawa na asilimia 20 kwa mwaka 2011.
Ndiye msanii wa kwanza Bongo kuchaguliwa kuwania tuzo za BET katika kipengele cha Best International Act, tayari amewania mara tatu (2014, 2016 na 2021) na kumfanya kuwa msanii pekee Bongo aliyewania mara nyingi.
Kwa kipindi cha miaka 12 katika muziki wa Bongofleva, Diamond ameweza kushinda na kutunukiwa tuzo zaidi ya 46 za ndani na za kimataifa, huku akimpiku Lady Jaydee mwenye tuzo zaidi ya 35.
Ndani ya muda huo ametoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018), pamoja na Extended Playlist (EP), First of All (2022), akiwa msanii pekee aliyefanikiwa kufanya hivyo.
Diamond ndiye msanii pekee katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara aliyevutia watazamaji zaidi ya bilioni 1.7 YouTube na kujikusanyia wafuasi zaidi ya milioni 6.3. Kumbuka mtandao huu unalipa wasanii, hivyo Diamond anaongoza kimauzo YouTube katika ukanda huo na sio Tanzania pekee.
Ikumbukwe albamu yake ya tatu ‘A Boy From Tandale’ ndio namba moja ya Bongofleva iliyosikilizwa zaidi kwenye mtandao wa Spotify ikiwa na wasikilizaji zaidi ya milioni 30.4. Inakadiriwa Spotify kulipa Dola 4,370 wastani wa Sh10.1 milioni kwa wasikilizaji milioni 1. Hadi sasa video ya wimbo wake ‘Nana’ inatajwa kama video ghali zaidi Bongo, iligharimu Dola 40,000 wastani wa Sh92.7 milioni, hakuna msanii Bongo aliyewahi kusema amefanya video zaidi ya bei hiyo, anafuatia na Alikiba ambaye video ya ngoma yake ‘Aje’ iligharimu Dola 32,000 wastani wa Sh74.2 milioni.
Kupitia lebo yake ya WCB Wasafi, wasanii anaowasimamia wamefanya vizuri, Rayvany ndiye msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo ya BET, huku Harmonize na Zuchu wakishinda tuzo ya Afrimma kama wasanii bora chipukizi pindi alipowatoa. Hakuna lebo Bongo imefanya hivi, tena ya msanii! Umaarufu wa kazi zake umemfanya kujizolea mamilioni ya wafuasi katika mitandao ya kijamii, ndiye msanii namba moja Tanzania na Afrika Mashariki upande huo katika mitandao mitatu mikubwa duniani, Instagram ana wafuasi milioni 14.2, Twitter milioni 1.1 na Facebook milioni 6.7. Kufikia mwaka 2018 Diamond alitambulika kama msanii wa kwanza nchini kumiliki vyombo vya habari, baada ya kuanzisha Wasafi Radio na TV, anatajwa kuwa msanii wa pili barani Afrika kufanya hivyo baada ya Youssou N’Dour wa Senegal.
Diamond pia ndiye msanii wa kwanza Tanzania kununua gari la kifahari aina Rolls-Royce Cullinan ambalo ametaja bei yake ni Sh2.2 bilioni, huku akililipia ushuru wa takribani Sh700 milioni. Na ndiye msanii wa kwanza Bongo kutangaza kutoza Sh162.2 milioni kwa shoo zake za kimataifa, huku akichukua Sh200 milioni kwa dili zake za ubalozi kila mwezi.
Apingwa kuzinanga tuzo za muziki nchini
Kutokana na hilo Mond amezikana tuzo za muziki zinazoandaliwa hapa nchini akisema wadau wa tuzo hizo ndiyo wamiliki wa redio zisizocheza nyimbo zake, hivyo ngumu kumpa tuzo.
Akihojiwa na kituo cha runinga cha Wasafi, staa huyo alisema, “Wameshindwa kunipa mirabaha, watanipa tuzo?”
Diamond alisema Tanzania haoni msanii wa kushindana naye, huku akitaka mshindi apatikane kwa kutazama anayefanya vizuri kimauzo mtandaoni.
Wakizungumza na kutoa maoni yao kuhusu kauli ya staa huyo, wasanii mbalimbali wamempinga wakidai kuwa kwao hizo tuzo zina heshima.
Miongoni mwa wasanii hao ni 20 Percent, mwenye rekodi ya kushinda tuzo tano kwa mpigo katika kinyang’anyilo cha KTMA. Anasema tuzo ni kwa ajili ya wote na sio wanaofanya vizuri mtandaoni, kwani hata wafuatiliaji wa muziki si wote wapo mitandaoni.
Kwa upande wa Afande Sele anasema mitandao iwe sehemu ndogo sana ya kumpata mshindi, kwani baadhi ya wasanii wanafanya udanganyifu akitolea mfano kile alichodia kununua watazamaji (viewers) YouTube.