Dar es Salaam. Baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuonekana akicheza wimbo Mwanza wa msanii Rayvanny ambao umefungiwa, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema kitendo hicho hakimaanishi kuwa wimbo huo umefunguliwa.
Novemba 12, 2018 Basata ilitangaza kuufungia wimbo huo wa Rayvanny aliomshirikisha mwanamuziki Diamond Platnumz kwa maelezo kuwa unahamasisha masuala yasiyokubalika katika jamii.
Baraza hilo lilieleza kuwa linawasiliana na mamlaka nyingine ili kuchukua hatua zaidi kwa kuwa tayari wimbo umeenea mitandaoni.
Siku chache baada ya kauli hiyo picha za video zimesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikimuonyesha Dk Tulia akicheza wimbo huo sambamba na watu wengine wakifurahia ushindi walioupata kwenye michezo.
Huku wakiimba mashairi ya wimbo huo, wameonekana wakifurahi na kutabasamu huku kila mmoja akionyesha ujuzi wake wa kusakata muziki hali iliyowafanya wavutie kuwatazama.
Akizungumzia suala hilo katibu wa Basata, Godfrey Mngereza amesema kitendo kilichofanywa na wabunge hao hakitengui uamuzi wa kufungiwa kwa wimbo huo kwa kuwa Basata wametekeleza wajibu wao kama wasimamizi wa sanaa.
“Kauli ya Basata haijabadilika kuhusu wimbo wa Mwanza kuwa haufai na umefungiwa. Kuhusu Wabunge sina cha kuongea kwani hawa ni viongozi wetu na mimi ni mtumishi wa Serikali. Baraza tumetimiza wajibu wetu," amesema Mngereza.