Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekana mashtaka yote 18 ya ufisadi anayokabiliwa nayo katika mahakama ya Pietermaritzburg nchini humo.
Akionekana mdhaifu na huku akiongea kwa utulivu, Jacob Zuma alisema anapinga makosa yote 18 ya ulaghai, ufisadi, ulaghai, ukwepaji wa kodi na utakatishaji fedha haramu.
Mashtaka hayo yanahusiana na matukio ya zaidi ya miongo miwili – katika siku za mwanzo za demokrasia ya Afrika Kusini – pamoja na mpango mkubwa wa silaha wenye utata.
Zuma na washirika wake wanasisitiza kuwa kesi hiyo ni ya kisiasa.Umati wa watu umekusanyika nje ya ukumbi wa mahakama huko Pietermaritzburg kuashiria kuwa Zuma bado ana umaarufu miongoni mwa wafuasi wake.
Zuma pia anakabiliwa na madai mapya ya ufisadi na huenda akafungwa jela kwa kukiuka amri ya mahakama katika kesi nyingine tofauti. Waafrika Kusini wanaamini kesi hiyo inaweza kuashiria mabadiliko ya nchi hiyo.
Baadhi ya mashujaa wa ukombozi wa Afrika Kusini walio hai wamemshtumu Zuma na kumlinganisha na jambazi na kuonya itachukua muda mrefu kurekebisha uharibifu alioufanya dhidi ya taasisi changa za nchi.