Zoezi la kuhesabu kura nchini Liberia linaendelea Jumatano, ili kuamua kama rais George Weah atashinda mhula wa pili baada duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika jana Jumanne.
Maafisa wa uchaguzi walianza kuhesabu kura Jumanne joini muda mfupi baada ya upigaji kura kumalizika.
Weah aliyewahi kuwa nyota wa kimataifa wa soka, mwaka 2017, alimshinda mpinzani wake Joseph Boakai kwenye duru ya pili ya uchaguzi, lakini matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa mwezi uliopita, yalionyesha wakiwa na matokeo yaliyokaribiana sana.
Katika wiki zilizofuata baada ya uchaguzi huo wa Oktoba 10, wote wawili walianza kuomba uungaji mkono kutoka kwa vyama vingine vya siasa.
Boakai alipata uungaji mkono wa vyama vilivyoshika nafasi za 3, 4 na 5 kwenye uchaguzi huo, suala ambalo huenda likapelekea ushindi wake kwenye duru ya pili. Weah kwa upande wake alipata uungaji mkono wa vyama viwili vya upinzani.