Zimbabwe ina mpango wa kuanzisha sheria ambayo itapiga marufuku Mataifa ya kigeni kuajiri wafanyakazi wake wa sekta ya afya.
Makamu wa Rais wa Zimbabwe Constantino Chiwenga ambaye pia ni Waziri wa Afya amesema kuchukuliwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na nchi zingine sasa kumekuwa sawa na biashara ya binadamu.
Chiwenga ameahidi kuweka adhabu kali kwa wale wote watakaohusika na kuiibia nchi hiyo nguvu kazi.
“Ikiwa mtu kwa makusudi kabisa ataajiri watu na kuifanya nchi yetu itaabike hii itakuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu. Watu wanakufa mahospitalini kwa sababu hakuna wauguzi na madaktari wa kutosha. Hii lazima tuichukulie kwa makini sana” alisema Chiwenga.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari zaidi ya wauguzi na madaktari 4,000 wameondoka nchini humo tangu mwezi Februari mwaka 2021.
Asilimia kubwa ya wafanyakazi hao huhamia Uingereza wakivutiwa na ukubwa wa mishahara.