Mama mmoja raia wa Zimbabwe amemuokoa mwanawe kutoka kwa mdomo wa nyani baada ya mnyama huyo kujaribu kumpokonya, aliiambia VOA (Voice of America).
Petronella Moyo alisema mtoto wake wa miezi 18 alikuwa akicheza nyumbani kwao Matabeleland wakati tukio hilo linatokea wiki iliyopita.
Alisema alimsikia mwanawe akipiga kelele na alipotazama juu, nyani huyo alikuwa akimburuta.
Nyani huyo aliruka juu ya nyumba huku mwanawe akining'inia mdomoni na akasema: "Niliogopa sana. Nilidhani amefariki".
Lakini alimkimbiza nyani huyo na kufanikiwa kumrudisha mtoto wake.
Mtoto wa Bi Moyo alipata majeraha machache lakini anatarajiwa kupata nafuu kamili katika Hospitali ya Mkoa wa Gwanda.
Nyani kwa ujumla hawana shughuli na binadamu, lakini hushambulia wanapokasirishwa, na wanaweza kuwa hatari sana kwa sababu ya meno na makucha yao makali.