Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zijue nchi sita ambazo vikosi vya ECOWAS viliingia kijeshi

Ecowas Vikosi Kijenshi.png Zijue nchi sita ambazo vikosi vya ECOWAS viliingia kijeshi

Wed, 9 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi Ecowas ilikuwa imeweka makataa ya siku saba kwa serikali ya kijeshi nchini Niger kujiondoa madarakani - venginevyo itakabiliwa na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi.

Baadhi ya vikwazo vimeidhinishwa dhidi ya viongozi hao na huduma ya kusambaza umeme kutoka Nigeria imekatwa, pamoja na kufungwa kwa mipaka, hatua inayomaanisha kuwa bidhaa hazitoingia katika nchi hiyo.

Amri ya Ecowas kwa majenerali wa kijeshi waliompindua rais Mohamed Bazoum, haijatiiwa - wanaendelea kung’ang’ania madaraka. Uamuzi wa Ecowas kutuma vikosi vya kijeshi katika nchi hiyo bado hauna uhakika.

Lenya uhakika ni kuwa – Ecowas ina historia ndefu ya kuingia kijeshi katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi kupitia jumuiya yake ya uangalizi ya kijeshi ya Ecomog. Ikiwa Ecowas itaamuru vikosi vipelekwe Niger, hilo ni la kusubiri na kuona. Liberia

Mwaka 1990, viongozi wa nchi za Afrika Magharibi walituma vikosi vya kijeshi nchini Liberia kuingilia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikosi vya rais wa wakati huo Samuel Doe na makundi ya waasi.

Vita vya kwanza vya wenyewe kwa wenye vilianza 1989 hadi 1997. Vita hivyo viliuwa takribani watu 200,000. Vita vya pili vya wenye kwa wenye vilianza 1999 hadi Octoba 2003, zaidi ya watu 250,000 waliuawa. Mara zote mbili Ecowas iliingia kijeshi kutuliza hali ya mambo. Sierra Leone

Mwaka 1998, kikosi cha Ecomog kikiongozwa na Nigeria kiliingilia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sierra Leone, ili kuindoa madarakani serikali ya kijeshi na makundi washirika ya waasi kutoka katika mji mkuu wa Freetown.

Walifanikiwa kumrejesha madarakani Rais Ahmad Tejan Kabbah, aliyekuwa ameondolewa madarakani katika mapinduzi mwaka mmoja uliopita. Mwaka 2000, kikosi hicho kiliondoka, na kukabidhi operesheni za kulinda amani kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Vita vya miaka kumi viliisha 2002. Guinea-Bissau

Mwaka 1999, Ecowas ilituma karibu wanajeshi 600 wa Ecomog kulinda makubaliano ya amani huko Guinea-Bissau. Waasi walichukua madaraka miezi mitatu baadaye na vikosi vya Ecowas vikalazimika kuondoka katika nchi hiyo.

Ecowas ilituma kikosi kingine 2012 hadi 2020, kusaidia kuzuia jeshi kuingilia siasa na kulinda viongozi wa kisiasa baada ya mapinduzi mengine kutokea. Ilituma kikosi kingine cha watu 631 mwaka 2022 kusaidia kuleta utulivu baada ya mapinduzi yaliyoshindwa. Ivory Coast

Kikosi cha kulinda amani cha Afrika Magharibi kilitumwa nchini Ivory Coast mwaka 2003. Wanajeshi 3,200 waliwasili Januari kusaidia vikosi vya Ufaransa kulinda amani. 2004 kikosi hicho kilijumuishwa katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

Vita vya wenyewe kwa wenye ulikuwa ni mgogoro ulioanza kwa uasi wa jeshi la nchi hiyo Septemba 2002. Uasi huo ulimalizika Machi 2007 baada ya msururu wa vikao ambavyo baadaye vilizalisha makubaliano ya amani. Mali

Ecowas ilituma wanajeshi nchini Mali mwaka 2013 kama sehemu ya misheni ya kuwafukuza wapiganaji wanaohusishwa na al Qaeda kaskazini mwa nchi hiyo. Kikosi hicho baadaye mwaka huo kilikabidhi operesheni hiyo kwa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Katika eneo la ukanda wa Sahel kuna makundi ya wapiganaji wa Kiislamu – wale wa al Qaeda na Dola la Kiislamu, ambao wamefurushwa Mashariki ya Kati baada ya kushindwa vita vilivyoongozwa na Marekani. Gambia

Mwaka 2017, Ecowas ilituma wanajeshi 7,000 nchini Gambia kutoka nchi jirani ya Senegal ili kumlazimisha Rais Yahya Jammeh kuachilia urais kwa Adama Barrow, ambaye alimshinda katika uchaguzi.

Vikosi vya usalama vya Jammeh havikutoa upinzani wowote kwa operesheni hiyo, ambayo ilipewa jina la Operesheni ya Kurejesha Demokrasia. Kwa sasa Jammeh anaishi uhamishoni katika nchi jirani ya Equatorial Guinea.

Tukio la sasa huko Niger limeacha mgawanyiko miongoni mwa nchi wanachama. Wakati mataifa mengi yako tayari kuingia kijeshi huko Niger; Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya hiyo anakabiliwa na upinzani mkubwa nchini mwake.

Fauka ya hilo, wanajeshi nchini Mali na Burkina Faso wameapa kuwatetea viongozi wa mapinduzi ya Niger iwapo Ecowas itatumia nguvu, hili linaongeza uwezekano wa kutokea kwa mzozo mkubwa wa kikanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live