Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchini Vatican, Deogratias Ndagano Mangokube, amesema ziara ya Papa Francis nchini DRC mwezi huu itafufua juhudi za amani kwa wanaotafuta amani kwa watu wa nchi hiyo.
Akizungumza baada ya hotuba ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani (Papa Francis) kwa jopo la wanadiplomasia, Balozi Ndagano aliiambia Vatican News kwamba, ziara ya Papa Francis nchini kwake kuanzia Januari 31, 2023 itakuwa uamsho na pumzi ya hewa mpya kwa maisha ya Wacongo.
Mwanadiplomasia huyo alimshukuru Papa Francis kwa ukaribu wake wa mara kwa mara kwa watu wanaoteseka nchini humo na vita inayoendelezwa na magenge ya watu yenye silaha, hasa katika eneo la Mashariki.
Kwa mujibu wa balozi huyo, katika hotuba yake kuu ya kila mwaka kwa wanadiplomasia, Papa alizungumzia maovu yanayoikumba dunia huku akitamani mwaka huu uwe wa uvumbuzi wa amani ulimwenguni.
Alisema kwa sasa hali ya mgawanyiko na vita inaonekana kuongezeka ulimwenguni.