Uwanja wa Taifa wa Mashujaa ambao ndio uwanja wa kisasa zaidi wa Zambia huko Lusaka, mji mkuu wa nchi hiyo na ambao uliteuliwa kuwa kituo cha taifa cha kutibu ugonjwa wa kipindupindu hivi sasa hauna tena wagonjwa huku kesi za ugonjwa huo zikidi kupungua.
Waziri wa Afya wa Zambia, Sylvia Masebo alitoa taarifa hiyo jana Ijumaa na kusema kuwa, kituo hicho ambacho wakati fulani kilikuwa na wagonjwa zaidi ya 1,000 hivi sasa hakina tena wagonjwa waliolazwa.
Waziri Masebo amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa: “Nina furaha kutangaza kuwa hatuna wagonjwa waliolazwa katika kituo chetu cha matibabu cha Taifa cha Uwanja wa Mashujaa. Tunajivunia na kufurahia kazi yetu ya pamoja na tunaweza kusherehekea maisha tuliyookoa katika kituo hiki wakati tulipofanya kazi kama watu wamoja dhidi ya adui wa pamoja.
Ameelezea furaha yake kutokana na kuendelea kupungua wagonjwa wa kipindupindu nchini humo ambapo kwa sasa ni wagonjwa 108 pekee waliolazwa katika vituo vya matibabu kote nchini humo. Wizara ya Afya ya Zambia imesema, kesi za ugonjwa wa kipindupindu zinazidi kupungua
Ameongeza kuwa, Zambia ilirekodi kesi 90 mpya katika kipindi saa 24 zilizopita na kifo kimoja. Aliwapongeza wahusika wote kwa juhudi zao za kupambana na ugonjwa huo lakini akaomba ushirikiano uendelee hadi pale ugonjwa huo utakapotokomezwa kikamilifu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Zambia imerekodi kesi 19,930, na vifo 686 na waliopona 19,136 tangu mripuko mpya wa kipindupindu ulipozuka nchni humo mwezi Oktoba mwaka jana.
Mwezi uliopita wa Januari, Wizara ya Afya ya Zambia ilitangaza kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu yamebainika katika karibu nusu ya wilaya zote za nchi hiyo na mikoa yake tisa kati ya 10.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyoi, kesi 400 mpya za watu walioambukizwa ugonjwa huo zilikuwa zinaripotiwa kila siku mwezi uliopita wa Januari huku idadi ya watu waliokuwa wamefariki dunia hadi wakati huo ikipindukia 400.