Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zambia: Simba waliosababisha shule za karibu na hifadhi kufungwa wauawa

Zambia: Simba Waliosababisha Shule Za Karibu Na Hifadhi Kufungwa Wauawa Zambia: Simba waliosababisha shule za karibu na hifadhi kufungwa wauawa

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Bbc

Mamlaka ya Zambia imewaua simba wawili ambao walizua hofu katika eneo la Zambezi magharibi, na kusababisha kiuanzishwa mipango ya kufunga shule zilizo karibu.

Simba hao wawili, wanasemekana kutoroka katika Hifadhi ya Kitaifa ya Kafue iliyo karibu, na kuua ng'ombe 16 katika muda wa wiki mbili.

Mkazi mmoja aliliambia shirika la utangazaji la serikali ZNBC baadhi ya watu walikuwa na wasiwasi kuhusu kuondoka kwenye nyumba zao.

Mamlaka ilikuwa imetangaza mpango wa kufunga baadhi ya shule katika eneo hilo kama tahadhari.

"Kuna hatari ya kweli kwamba wanafunzi wanaweza kushambuliwa wakiwa njiani kwenda shule," mkuu wa wilaya, Simeon Machayi, alikuwa amenukuliwa akisema.

"Ili kulinda maisha ya binadamu, baadhi ya shule katika eneo hilo zitafungwa kama hatua ya tahadhari," alisema.

Wakati simba hao walikuwa wameshambulia mifugo pekee, mamlaka ilisema walihatarisha maisha ya binadamu.

Gazeti la Lusaka Times lilisema kisa cha hivi karibunu zaidi ni shambulio dhidi ya mkokoteni wa ng'ombe uliokuwa umebeba mgonjwa hadi Hospitali ya Wilaya ya Zambezi siku ya Jumanne.

Inasemekana kulikuwa na hali ya afueni wakati polisi na mamlaka ya wanyamapori walipoingia kushughulikia suala hilo siku ya Jumatano.

"Mioyo yetu sasa imetulia," mkuu wa wilaya alisema. Mtangazaji wa serikali Jumatano alionesha mizoga ya simba hao wakubwa, na umati mkubwa wa watu wenye furaha ambao walikuwa wamekusanyika.

Mwalimu alisema sasa walikuwa na furaha kuanza maisha yao bila woga, akisema wanafunzi na walimu wamekuwa "wakiogopa sana kufanya harakati zao" katika eneo hilo.

Migogoro kati ya watu na wanyamapori ni ya kawaida nchini Zambia haswa miongoni mwa jamii zinazoishi karibu na mbuga na hifadhi za wanyamapori.

Hali hiyo imechangiwa na ukame ambao umepunguza chanzo cha chakula cha watu na wanyama.

Chanzo: Bbc