Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni nne wameyakimbia makaazi yao nchini Ethiopia kutokana na mzozo na ukame katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Ripoti ya Shirika la Wahamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, kuhusiana na watu wanaoyakimbia makaazi yao nchini humo imesema jumla ya watu milioni 4.38 wameyakimbia makaazi yao kuanzia Disemba 2022 hadi Juni 2023 mwaka huu.
Kulingana na ripoti hiyo mizozo iliongoza kwa kuchochea tatizo hilo kwa asilimia 66.41 huku janga la ukame likichangia kwa asilimia 18.49.
Zaidi ya watu milioni moja waliukimbia mkoa wa Tigray uliokumbwa na machafuko.
Jumla ya watu milioni 28 nchini Ethiopia wanahitaji msaada, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za umoja huo.
Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2021 ripoti hiyo imeangazia eneo lililokumbwa na vita la Tigray, ambako idadi kubwa ya raia wa Ethiopia walipateza makazi yao kutokana na vita, idadi hiyo ikitajwa kuwa zaidi ya watu milioni moja.
Eneo la Somali mashariki mwa Ethiopia linakaliwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana baa la ukame.
Hapo awali Umoja wa Mataifa ulikuwa imeeleza kuwa, zaidi ya raia wa Ethiopia milioni 20 walikuwa wakihitaji msaada wa chakula ambapo dola bilioni nne zilihitajika kukidhi mahitaji yao.
Mapema mwezi huu, mapigano makali yalizuka kati ya Jeshi la Ethiopia (ENDF) na wanamgambo wa eneo la Fano wa Amhara juu ya uamuzi wa serikali wa kuunganisha vikosi vya kikanda katika polisi wa shirikisho au jeshi.
Serikali ilitangaza hali ya hatari ya miezi sita wiki iliyopita ili kukabiliana na ghasia zilizotokea Bahir Dar, Gondar, mji wa kihistoria wa Lalibela na miji mingine, ambazo zimesababisha vifo vya raia kadhaa.