Umoja wa Mataifa Jumanne umesema kwamba ghasia za Sudan huenda zikapelekea zaidi ya wakimbizi milioni 1 kuondoka kwenye taifa hilo la Afrika kufikia Oktoba, wakati mapigano yaliochukua takriban wiki 10 yakionyesha dalili chache za kumalizika.
Sudan ilitumbukia kwenye ghasia baada ya mapigano kuzuka katikati mwa mwezi Aprili kati ya jeshi la serikali likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah Burhan na kiongozi wa kikosi cha Rapid Support Forces, RSF, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Tangu wakati huo, zaidi ya watu 3,000 wameuwawa, kulingana na wizara ya afya ya Sudan, wakati takriban watu milioni 2 na nusu wakiwa wamekoseshwa makazi, kulingana na UN.
Mapigano makali yameshuhudiwa kwenye mji mkuu wa Khartoum lakini pia kwenye eneo la magharibi la Darfur ambapo RSF na wapiganaji wa kiarabu wanasemekana kulenga makabila yasiyo ya kiarabu, kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu na UN.
Wengi wa wakazi waliotoroka wameelekea nchini Chad upande wa mashariki.