Ofisi ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema Jumatano kwamba takriban watu 21 wakiwemo watoto 6 wamekufa kutokana na mafuriko nchini Somalia ndani ya wiki moja iliyopita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP,karibu watu laki moja wameathiriwa na mvua kubwa pamoja na mafuriko kwenye wilaya ya Bardhere iliyokuwa ikishuhudia ukame hivi karibuni kusini mwa taifa hilo kwenye mkoa wa Gedo.
Eneo lenye mafuriko ni karibu na Ethiopia ambako kumekuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha ongezeko kubwa la maji kwenye mito ya Shebelle na Juba. Idara ya kitaifa ya majanga ya Somalia imesema Jumatano kwamba vituo vya afya pia vimeharibiwa na mafuriko hayo.
Mshauri wa Idara hiyo Mohamed Moalim ameiambia AP kwamba jamii zinazoishi karibu na mito hiyo zimearifiwa kuhusu hatari iliyopo. Takriban familia 250 kwenye wilaya ya Bardhere zimampokea misaada ya chakula kutoka kwenye idara ya kitaifa ya dharura.