Mwanaume mmoja, Paul Murage Njuki (35), mkazi wa Kijiji cha Kathata, Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe, Millicent Muthoni na wanaye wanne kwa kuwakata na shoka.
Kamanda wa Polisi wa Gichugu, Anthony Mbogo, ameeleza kwamba baada ya kutekeleza ukatili huo, mwanaume huyo alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Kianyaga ambapo aliwaeleza polisi kwamba ameamua kujisalimisha kwa kuwa amekuwa akifanya biashara ya kuuza bangi, na kutaka afungwe miezi sita jela.
Kamanda huyo wa polisi, anasema alipopata taarifa hizo, alipatwa na mshangao na kuwaagiza askari wake wamchunguze kwa kina mwanaume huyo na hapo ndipo ilipogundulika kwamba kumbe alikuwa amemuua mkewe na wanaye wanne.
Baada ya kubanwa na maafisa wa polisi, mwanaume huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo na kueleza kwamba alianza kumuua mkewe, kisha ndipo akafuatia kuwaua wanaye hao ambao wana umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka 13.
Kamanda Mbogo ameeleza kwamba mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kianyaga na miili ya marehemu hao, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Kerugoya ikisubiri kufanyiwa uchunguzi.