Mwaka wa 2023 ulikuwa na mambo mengi sana, lakini pia ulikuwa na matukio mengi ya kushangaza ikiwemo tukio la Mchungaji Paul Mackenzie la mfungo tata na vifo vya waumini wake, matetemeko ya ardhi, vita, machafuko, mafuriko na hata mauaji, kiasi nikakumbuka kauli ya inayosema, “kuishi ni bahati.”
Lakini kubwa ambalo linachekesha na kusikistisha pia ni lile la Mchungaji Eliud Wekesa, maarufu kama Yesu wa Tongaren raia wa Magharibi mwa Taifa la Kenya, ambaye alijisalimisha Polisi kwa mahojiano baada ya kutakiwa kufanya hivyo ikiwa ni hatua mojawapo ya Serikali ya nchi hiyo kuwadhibiti wahubiri wenye misimamo na itikadi kali.
Siku moja baadaye, akapandishwa Mahakamani mjini Bungoma kwa tuhuma za kutiliwa shaka kwa mafundisho yake ya kidini, huku yeye akijitetea kuwa hana hatia na kwamba anafanya kazi ya kueneza injili kwa viumbe waliopotea na aksisitiza kwamba yeye ndiye Yesu.
Hata hivyo hakuaminika na akawekwa kizuizini kwa siku nne zaidi, ili kutoa nafasi kwa uchunguzi dhidi yake wakati vyombo vya usalama vikifuatilia mafunzo yake yanayodaiwa kuwa ni potofu yanayotolewa katika kanisa lake na yenye kuzusha taharuki na akapata Wakili wa kumtetea.
Katika mwendelezo wa kesi Wakili wa Wekesa alihoji kuwa kama mteja wake si Yesu na wapelelezi hawaamini basi anaomba wamlete Yesu halisi mbele ya Mahakama, jambo ambalo lilishindikana na hivyo kupelekea siku ya hukumu kupangwa kwa ajili ya kuhitimisha shauri hilo lililozua hisia miongoni mwa wakenya na Dunia kwa ujumla.
Hatimaye siku ikawadia na Yesu huyo (Wekesa), akapandishwa tena kizimbani kwa ajili ya hukumu mbele ya Mahakama ya Bungoma, Hakimu Mkuu Tom Olando akamwachilia huru bila vikwazo, akisema upande wa upelezi wa makosa ya jinai (Ofisi ya DCI), wamekosa ushahidi dhidi yake na kwamba mtuhumiwa hana kesi ya kujibu.
Hakika inatafakarisha, inashangaza na bile sheria huenda mambo yangekuwa tofauti, nadhani kinachotakiwa hapa ni namna ya kuchuja kile mtu anachodhani ni bora kwake na kwa jamii kiujumla kwa kuhusisha watu wenye hekima kupata muafaka, kwani bila umakini na bila kufanya tathmini ya mambo, ni wazi kuwa tutaangamia kama maandiko ya vitabu vya Dini zote yanavyotufundisha, TUWE MAKINI.