Orodha ya nchi zinazowaondoa raia wake na wanadiplomasia kutoka nchini Sudan inazidi kuongezeka huku mapigano makali yakiendelea kushika kasi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Siku ya Jumapili Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania zilitangaza kuwa zimewasafirisha wanadiplomasia na familia zao kutoka nchini humo ili kuwalinda dhidi ya mapigano hayo.
Mamlaka ya Marekani imesema kuwa imewasafirisha kwa ndege chini ya watu 100 na helikopta tatu za Chinook Jumapili asubuhi katika operesheni ya kuwaondoa nchini humo huku ubalozi wa Marekani mjini Khartoum ukiwa umefungwa.
Mapambano makali ya madaraka kati ya jeshi la kawaida na kikosi chenye nguvu yamesababisha ghasia kote nchini humo huku idadi ya waliopoteza maisha ikiripotiwa kufika 400 na baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa na kusababisha ukosefu wa baadhi ya mahitaji ikiwemo chakula.
Siku chache kabla ya mapigano kuanza, jeshi lilitoa tahadhari kwa raia wake kuweka akiba ya chakula kufuatia mapigano hayo katika maeneo tofauti ya mji mkuu.