Takriban wapiga kura 847,000 waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katika uchaguzi mkuu wa jana Jumamosi nchini Gabon.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, katika baadhi ya maeneo zoezi la upigaji kura lilichelewa sana kuanza hasa katika maeneo ya mji mkuu Libreville.
Wapiga kura mbalimbali waliohojiwa na waandishi wa habari wamesema kuwa, walikaa kwa zaidi ya saa 6 kusubiri kufunguliwa vituo vya kupigia kura.
Mmoja wa wapiga kura hao aliyejitambulisha kwa jina la Georges Bekale amewaambia waandishi wa habari kwamba amekaa kituoni kwa zaidi ya saa sita Alisema hayo akiwa mbele ya kituo kimoja cha kupigia kura huko Belle Vue ambayo ni Wilaya ya 3 ya mji mkuu Libreville.
Matatizo na usumbufu kama huo umeripotiwa pia katika miji kadhaa ya Gabon kama vile Port-Gentil ambao ndio mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo.
Rais Ali Bongo wa Gabon
Gabon imeitisha chaguzi tatu kwa siku moja, yaani uchaguzi wa rais, wabunge na serikali za mitaa. Wagombea 19 wamechuana kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka huu. Rais Ali Bongo Ondimba, wa chama tawala cha Gabon Democratic Party (PDG), ameshiriki kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo akipambana na wagombea wengine 18.
Takriban vituo 3,000 vya kupigia kura vimetengwa ndani na nje ya nchi hiyo. Takriban raia 16,000 wa Gabon waishio nje ya nchi wameidhinishwa kupiga kura lakini katika uchaguzi wa rais tu. Kwa mujibu wa Katiba ya Gabon, vituo vya kupigia kura vinapaswa kufungwa rasmi saa kumi na mbili jioni, kwa majira ya nchi hiyo.
Mipaka ya nchi kavu na baharini, pamoja na maeneo ya starehe yalifungwa jana Siku ya Uchaguzi ili kuhakikisha upigaji kura unafanyika kwa amani na utulivu.