Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ya Tunisia, Afrika Kusini yapo Afrika yote

7a9b5694b8f960c789b718049030acc1 Ya Tunisia, Afrika Kusini yapo Afrika yote

Wed, 11 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCHI ya Tunisia ipo katika mzozo wa kiuongozi kufuatia Rais wa nchi hiyo, Kais Saied, kumuengua Waziri Mkuu, Hichem Mechichi na mawaziri wengine wawili.

Hatua hiyo ilitokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kushindwa kusimamia vema ugonjwa wa uviko 19 na kusababisha maandamano makubwa jijini Tunis.

Swali hapa ni je ni kweli kuwa uviko 19 ndiyo kisababishi cha maandamano?

Kwa upande mwingine mwezi Julai dunia ilishuhudia vurugu kubwa na uvunjwaji wa maduka na makundi ya vijana nchini Afrika Kusini kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kupinga kufungwa kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.

Jambo la kujiuliza hapa ni kuwa kwa nini waandamanaji wasiende gerezani ambako amefungwa kipenzi chao badala yake wakaenda kuvunja maduka na kuiba vyakula na vinywaji?

Kwa nini waliiba vyakula na vinywaji na si vitabu?

Tukitazama matukio haya mawili ya Tunisia na Afrika Kusini tunaweza kubaini kuwa Afrika ina tatizo moja kubwa ambalo nchi nyingi zinakabiliwa nalo ingawa si nchi zote. Tatizo hili ni lipi?

Tatizo la Afrika lilipata kugusiwa katika Ripoti ya Berg ya mwaka 1981 Accerelated Development in Sub-Saharan Africa: A Plan for Action, kwamba tatizo la Afrika ni Utawala.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Utawala (Governance) ni namna ambavyo mamlaka na madaraka yanatumika katika kusimamia vema uchumi wa nchi na rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo ya nchi husika.

Kwa maana nyingine ni kwamba tatizo kubwa la Afrika ni kukosa usimamizi mzuri wa uchumi na rasilimali kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Paul Collier katika andiko lake; Wars, Guns, and Votes: Democracy in Dangerous places la mwaka 2009 anakazia kwa kusema, 'wakati rasilimali zina nafasi kubwa ya kusaidia kuleta maendeleo Afrika, zimekuwa zikisaidia pia kuchochea migogoro.'

Sasa kwa nini nimesema matatizo yanayojiri Tunisia na Afrika Kusini yanaakisi asilimia kubwa ya nchi za Afrika?

Ni kwamba kwa mujibu wa OECD, kukosekana utawala unaokidhi matakwa ya wananchi husababisha kuwepo kwa mambo manne ambayo ni kukosekana kwa uwajibikaji, kukosekana kwa uwazi, kukosekana kwa utawala wa sheria na hatimaye kutamalaki kwa rushwa (Rejea Managing Development: The Governance Dimension, Discussion Paper, World Bank, 1991).

Kilichojiri Tunisia na Afrika Kusini ni zao la kukosekana kwa utawala thabiti.

Sasa tujiulize, Jacob Zuma hakuwa na kesi ya rushwa, hatusikii nchi nyingine za Afrika zikilalamikiwa kuwa na rushwa iliyotamalaki?

Wananchi wa Tunisia sasa wanaingiwa na hofu kuwa kitendo Rais Kais kulisimamisha Bunge amevunja utawala wa sheria na anairejesha nchi hiyo kwenye utawala wa Ben Ali ambaye alichukuliwa kama dikteta.

Je, hatujapata kushuhudia mizozo ya Bunge na Serikali katika nchi kama Ethiopia, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)?

Lakini kipekee, kukosekana kwa usimamizi mzuri wa uchumi na rasilimali ndiko kumesababisha kuwepo kwa kundi kubwa la vijana nchini Tunisia ambao hawana ajira?

Usimamizi dhaifu wa rasilimali ni aina mpya ya kitisho cha kiusalama kinacholikabili bara la Afrika (Rejea andiko la Paul Collier, Security Threats Facing Africa and its Capacity to Respond).

Kimsingi, kukikosekana usimamizi na mgawanyo mzuri wa rasilimali husababisha kutokea kwa mgawanyiko mkubwa wa kipato kati ya walio nacho na wasio nacho na hivyo kundi la wasio nacho kujikuta limetengwa (marginalized) katika keki ya taifa na maendeleo na hivyo kusababisha umasiki mkubwa kwa kundi hilo. Rejea andiko la Mondal (2018) Poverty, Politics and the Socially Marginalized-a state level analysis in India.

Hata Badru (1991:220) alibainisha kuwa chanzo kikuu cha mgogoro usioisha nchini Ethiopia ni kutengwa (marginalization) kwa baadhi ya jamii katika maendeleo ya kiuchumi.

Kwa Tunisia jamii ya vijana imetengwa katika maendeleo kwa kukosa ajira na hili lipo nchi nyingi Afrika, lakini pia Tunisia inakabiliwa na tatizo la rushwa lililotamalaki hivyo corona si suala lililowafanya vijana wale waandamane bali corona kwao ilikuwa kisababishi (immediate cause) cha wao kuonesha hisia zao za kutengwa kwa kukosa ajira.

Tukumbuke Desemba 18 mwaka 2010, kijana aliyemaliza chuo kikuu, Mohamed Bouazizi kutoka mji wa Sidi Bouzid aliyekuwa akiuza mbogamboga alijimwagia mafuta na kujichoma moto kupinga tabia ya polisi kuchukua rushwa na kuwanyanyasa wafanyabiashara kama yeye.

Hatua yake hiyo ilisababisha kile kilichoitwa kama vuguvugu la mabadiliko katika nchi za kiarabu yaani Arab Spring. Je, kuna tofauti kati ya maandamano yale na haya ya juzi kwa kuangalia sababu halisi?

Kwa Afrika Kusini vivyo hivyo, iweje Zuma amefungwa gerezani wao wakavunje maduka?

Hapa tunagundua kuwa kwao suala si Zuma kufungwa bali umaskini uliokithiri ndiyo tatizo, na ndiyo maana wakawahi kuiba vyakula na si vitabu.

Utawala nchini Afrika Kusini umeshindwa kuondoa tofauti ya kipato kati ya walio nacho (weupe) na wasio nacho (weusi) hivyo kusababisha watu weusi kujiona wametengwa katika keki ya taifa.

Hivyo hili ni suala la kisera, kiuongozi na kiutawala kushindwa kutafuta namna ya kufanya uchumi kuwa jumuishi kwa watu wote kama ambavyo DESA (2019) walivyopata kubainisha.

Bila ya kuwa na Sera ya kutafuta namna ya kulihusisha kundi hili la vijana wanaovunja maduka katika keki ya taifa kila litakalotokea watalitumia kama mwanya wa kuandamana na kuvunja maduka. Sote tunakumbuka chuki dhidi ya watu weusi (xenophobia) ambayo ni zao la kukosa ajira na umasikini uliokithiri zilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Katika hili Aliyu na wenzake katika andiko lao la mwaka 2018 'Poverty: A Threat to Good Governance and Security in Africa' walikazia haya yaliyotokea Afrika Kusini kwa kusema, "Wananchi wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri Afrika hawaonekani kukumbatia sera za Serikali endapo tu mahitaji yao ya msingi kama vile malazi (makazi), mavazi na chakula hayajatimizwa ipasavyo.

Ndiyo maana wanafalsafa wa zamani walipata kusema, 'A hungry man is an angry man' kwa tafsiri yangu isiyo sahihi ni kuwa 'Mtu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira.' Nao wajuzi wa Kiswahili wakasema 'Njaa haimpendezi mtu' haya yote yanatoa picha ya namna gani kukosekana kwa utawala bora husababisha matatizo makubwa katika nchi husika.

Haya pia unaweza kuyaona katika andiko la Rjoub na wenzake saba la mwaka huu 2021 lenye kichwa 'Implications of Governance, Natural Resources, and Security Threats on Economic Development: Evidence from Sub-Saharan Africa' na kubaini ukweli huu.

Hivyo kwa ujumla yanayojiri Tunisia na Afrika Kusini yanaakisi hali ya Utawala kwa asilimia kubwa ya nchi za Afrika.

NINI KIFANYIKE?

Serikali za Afrika zinapaswa kujielekeza katika kutatua matatizo ya msingi ya wananchi kama vile afya,hospitali, maji safi na salama, elimu, barabara, usafiri, sambamba na kuweka miundombinu ya kuwawezesha wananchi kujiajiri,na mazingira wezeshi ya biashara, uwekezaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz