Wimbi jipya la machafuko kaskazini mwa Msumbiji, eneo linaloshuhudia uasi wa wanajihadi, limewalazimu maelfu kukimbia makazi yao, kulingana na takwimu na vyanzo vya Umoja wa Mataifa katika jimbo la Cabo Delgado.
Tahadhari kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM ilisema mashambulizi ya hivi karibuni katika wilaya za Macomia, Chiure na Mecufi, yamewakosesha makazi watu 13,088 -- wengi wao wakiwa watoto – baadhi wakitoroka kwa basi, mitumbwi na kwa miguu.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alithibitisha kumekuwa na wimbi jipya la watu wanaotoroka, lakini alipuuzilia mbali dhana hiyo na kusisitiza kuwa vikosi vya usalama vimedhibiti hali hiyo.
"Kuna idadi kubwa ya watu wanaohama kutoka eneo moja hadi jingine na kulalamikia kuhusu kukosa usaidizi," alisema Nyusi, baada ya mkutano na makamanda wa kijeshi.
Wimbi la hivi karibuni la watu kutoka mji wa Ocua, alisema, lilitokana na mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya vikosi vya Msumbiji na Rwanda kuzuia jaribio la kuwateka nyara watoto.