Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov amezulu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea nchi za Afrika kwa ajili ya kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo nan chi yake ya Urusi.
Lavrov anatembelea mataifa ya Afrika ambayo yamekuwa na uhusiano mzuri na Urusi na yasiyofungamana na upande wowote kwa Mataifa ya Ulaya na hasa linapokuja suala la vita kati ya Urusi na Ukraine.
Mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakinufaika na misaada kutoka kwa Mataifa ya Magharibi lakini pia yakinufaika na kupokea bidhaa za nafaka kutoka Ukraine na Urusi.
Taarifa zinadai Lavrov tayari ameshatembelea nchi ya Misri na baada ya kutoka Congo atatembelea nchi ya Uganda kisha atamalizia ziara yake katika Taifa la Ethiopia ambako ndiko yaliko Makao Makuu ya Umoja wa Afrika AU.
Aidha mbali na ziara ya Lavrov nchi za Bara la Afrika pia zinatarajiwa kutembelewa na Rais wa sasa wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye anatajwa kuzuru katika mataifa ya Cameroon, Benin Pamoja na Guinnea-Bissau huku pia ujumbe kutoka Marekani chini ya Mike Hammer ukitarajiwa kutembelea mataifa ya Misri Pamoja na Ethiopia.
Inaelezwa kuwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa na uhusiano mzuri na Urusi ambapo kwa miaka mingi ameweza kumudu kuweka sawa uhusiano wa Urusi Pamoja na Mataifa mengine ya Magharibi ingawa kwa sasa duru za kiintelijensia zimebainisha kuwa Rais Museveni amewekeza nguvu kubwa katika kuimarisha uhusiano wake na taifa la Urusi ambao wameonekana kuunga mkono utawala wake tofauti na mataifa ya magharibi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni wameonekana kukosoa mfumo wa utawala pamoja na Demokrasia nchini Uganda.