Waziri mkuu wa zamani wa Burundi mwenye ushawishi mkubwa Alain Guillaume Bunyoni alifikishwa mahakamani Jumatatu akituhumiwa kuhatarisha usalama wa taifa na kumkashifu rais, chanzo cha mahakama na mashahidi walisema.
Bunyoni alikuwa waziri mkuu kuanzia katikati ya mwaka 2020 hadi Septemba 2022, lakini alifutwa kazi baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuchukua hatamu za uongozi.
Bunyoni ambaye ni mkuu wa zamani wa polisi na waziri wa zamani wa usalama wa ndani, nafasi yake ya waziri mkuu ilichukuliwa na waziri wa mambo ya ndani wa wakati huo Gervais Ndirakobuca, siku chache baada ya Ndayishimiye kuonya juu “ ya njama” ya kumuondoa madarakani.
Alikamatwa mwezi uliopita mjini Bujumbura.
Bunyoni Jumatatu alisikilizwa na jopo la majaji wa kitengo cha mahakama ya juu ambao waliamua awekwe kizuizini katika jela ya mkoa wa kaskazini mwa Burundi wa Ngozi kabla ya kesi yake kuanza, chanzo cha mahakama ambacho kimeomba jina lake lihifadhiwe kimeiambia AFP.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa waziri huyo mkuu wa zamani alishtakiwa siku ya Ijumaa mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama ya juu katika kikao cha faragha.
Bunyoni anatuhumiwa “kuhatarisha usalama wa taifa, kuhujumu uchumi wa taifa na kupata utajiri kwa njia haramu”, kulingana na nyaraka za mahakama ambazo shirika la habari la AFP imeziona.
Anakabiliwa pia na mashtaka ya kumliki silaha kinyume cha sheria na kumkashifu rais.